Habari za Kitaifa

Hatimaye Raila akohoa kuhusu Mswada wa Fedha wa 2024

June 7th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa Orange Democratic Movement (ODM) Raila Odinga amependekeza kuwa Mswada wa Fedha wa 2014 ufanyiwe mageuzi kwa sababu ukipitishwa jinsi ulivyo utawaumiza Wakenya.

Kwenye taarifa aliyoitoa Ijumaa jioni, Bw Odinga alisema mapendekezo mengi kuhusu utozaji ushuru yaliyo katika mswada huo “ni mabaya kwani hayazingatii masilahi ya wananchi wa kawaida”.

“Mswada wa Fedha wa 2024 unapendekeza mfumo wa utozaji ushuru ambao hautabiriki, ni ngumu kuuelewa, hauna uwazi na hauzingatii usawa na haki. Kwa hivyo ni vigumu kutekelezwa,” akaeleza Bw Odinga.

“Mswada huu ni mbaya kuliko ule wa 2023, utaua uwekezaji na unaongeza machungu kwa Wakenya ambao walitarajia kuwa machozi yaliyowatoka kuhusiana na ushuru wa mwaka 2023 yangeisukuma serikali kuwapunguzia mzigo wa ushuru mwaka huu wa 2024,” akasema.

Mswada huo ambao tayari umepingwa na wadau katika sekta mbalimbali za uchumi na Wakenya wa kawaida, umependekeza aina mbalimbali za ushuru kuiwezesha serikali kukusanya mapato ya ziada ya Sh302 bilioni katika mwaka wa kifedha wa 2024/2025.

Kwa ujumla, serikali inalenga kukusanya mapato ya kima cha Sh3.35 trilioni katika mwaka huo wa kifedha unaoanza Julai 1, 2024.

Miongoni mwa kategoria za ushuru zinazopendekezwa katika mswada huo ni ushuru wa ziada ya thamani ya asilimia 16 kwa mkate, ushuru wa asilimia 20 kwa mafuta ya kupikia, nyongeza ya ushuru unaotozwa hudumu za kupokea na kutuma pesa kwa njia ya simu kutoka asimilia 10 hadi asilimia 20, na ushuru wa magari wa asimilia 2.5 miongoni mwa nyingine.

“Kuongezwa kwa ushuru wa kutuma na kupokea pesa kutaongeza gharama ya huduma hiyo inayotegemewa na Wakenya wengi sawa na nyongeza ya ushuru kwa bidhaa za kimsingi kama mkate na mafuta ya kupikia,” akaeleza.

Waziri huyo mkuu wa zamani, ambaye pia ni kiongozi wa ODM, alisema kuwa mapendekezo ya ushuru kwenye mswada huo yatawaumiza Wakenya maskini ambao tayari wanaumizwa na kategoria za ushuru zilizoko kwenye Sheria ya Fedha ya 2023.

Aina nyingine za ushuru ambazo Bw Odinga anapinga ni ushuru kwa ‘diapers’ zinazotumika na akina mama waliojifungua.

“Kwa hivyo wabunge wanapaswa kuyafanyia mageuzi mapendekezo ya ushuru katika Mswada wa Fedha wa 2024. Hatutakubali makosa na machungu ambayo Wakenya wanapitia chini ya Sheria ya Fedha ya 2023 yaendelezwe hadi 2025 kupitia Mswada wa Fedha wa 2024,” Bw Odinga akaeleza.