Raila ana sapoti ya marais wa EAC, Ruto afichulia wabunge EALA
NA CHARLES WASONGA
RAIS William Ruto amesema marais wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wamekubaliana kuunga mkono mgombeaji mmoja katika kinyang’anyiro cha uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).
Akiongea Jumanne alipofungua rasmi kikao cha tatu cha Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) katika Majengo ya Bunge jijini Nairobi, Dkt Ruto alisema makubaliano hayo ni kielelezo cha nguvu na uthabiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Aliongeza kuwa muafaka huo pia unaonyesha moyo wa “umoja wa uongozi” ulioko katika mataifa wanachama wa EAC.
“Uchaguzi wa mwenyekiti wa AU utafanyika mwaka 2025 kwani kipindi cha kuhudumu kwa mwenyekiti wa sasa Moussa Mahamat Faki unakamilika. Wakati huu itakuwa ni zamu ya Afrika Mashariki kutoa mwenyekiti wa AUC,” Dkt Ruto akasema.
“Tumeketi chini kwa moyo wa EAC, tumeshauriana kama marais wa mataifa wanachama wa jumuiya hii na kukubaliana kumdhamini mgombeaji mmoja. Huo ndio umoja na nguvu yetu… kwamba tunaweza kushauriana na kufanya vitu pamoja. Ni kielelezo tosha cha aina ya uongozi bora ulioko katika eneo letu,” akaongeza.
Serikali ya Kenya imemdhamini kiongozi wa Azimio La Umoja-One Kenya Raila Odinga kama mgombeaji wa kiti hicho cha AUC.
Tayari serikali imebuni kikosi kinachoongozwa na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi kumfanyika Bw Odinga kampeni katika mataifa yote 54 ya Afrika ambayo ni wanachama wa Umoja wa Afrika.
Hata hivyo, wiki jana aliyekuwa Waziri wa Masuala ya Kigeni wa Somalia Fawzia Yusuf Adam alitangaza azma yake ya kuwania wadhifa wa AUC.
Bi Adam, ambaye ni mwanamke wa kwanza kushikilia wadhifa wa Waziri wa Masuala ya Kigeni Somalia, mnamo Jumatano wiki jana alisema kwamba amepata uungwaji mkono kutoka kwa serikali ya Rais Hassan Sheikh Mohamud.
“Nitataka kupaza sauti ya Afrika na kuendeleza ajenda ya bara hili lenye utajiri mkubwa,” Bi Adam akanukuliwa akisema.
Msemaji wa serikali ya Somalia na Waziri wa Habari Daud Aweis alikariri kuwa serikali ya nchi hiyo itamuunga mkono Bi Adam kwa sababu ni mwamko mpya kwa taifa hilo katika rubaa za kimataifa.
“Kufuatia mafanikio ya kidiplomasia kama vile kuondolewa kwa vikwazo vya silaha, msamaha wa madeni na kujiunga na jumuiya ya Afrika Mashariki, Somalia sasa iko katika nafasi nzuri ya kutoa mchango wake katika ngazi za ulimwengu,” Bw Aweis akasema.
Somalia ilijiunga rasmi na jumuiya ya EAC Jumatatu wiki hii baada ya kuwasilisha stakabadhi zake rasmi katika makao makuu ya jumuiya hiyo jijini Arusha, Tanzania.
Bw Odinga ambaye alitangaza rasmi azma yake ya kuwania wadhifa wa AUC mnamo Februari 15, 2024, amepata uungwaji mkono kutoka mirengo yote ya kisiasa nchini.
Aidha, duru zasema kuwa amepata uungwaji mkono kutoka kwa baadhi ya marais wa mataifa wanachama wa EAC.
Kando na Rais Ruto wengine ni Yoweri Museveni (Uganda), Samia Suluhu Hassan (Tanzania) na Paul Kagame wa Rwanda.