Habari za Kitaifa

Raila anakumbukwa kwa kupigania mageuzi mengi nchini

Na SAMWEL OWINO October 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HAYATI Raila Odinga atakumbukwa kama nguzo ya mageuzi makubwa nchini Kenya.

Mwanasiasa huyo mashuhuri nchini na ulimwenguni aliyefariki jana nchini India alikoenda kutibiwa, atakumbukwa kama shujaa wa mageuzi wa kikatiba, demokrasia ya vyama vingi na mtetezi wa haki kwa wote.

Odinga, aliyeaga dunia akiwa na umri wa miaka 80, alionyesha kujitolea kwake kupigania utawala wa kidemokrasia na mageuzi, kiasi cha kujitolea kupoteza kisiasa na hata kuweka maisha yake hatarini.

Anakumbukwa kwa kuwa mwanasiasa wa kipekee aliyefungwa jela kwa miaka minane, bila kufunguliwa mashtaka wakati wa utawala wa Rais wa zamani, Daniel Toroitich Arap Moi.

Mnamo 1991, Raila alitambuliwa na Shirika la kutetea haki, Amnesty International kwa mchango wake katika utetezi wa utawala wa vyama vingi vya kisiasa na mageuzi ya kikatiba.

Katika taarifa jana, shirika hilo lilisema uanaharakati wa Bw Odinga na ukakamavu wake ulichangia kuchipuka kwa makundi ya kutetea haki za kibinadamu nchini Kenya na bara la Afrika kwa ujumla.

“Katika maisha yake ya kisiasa yaliyodumu kwa miongo minne, Odinga aliendelea kutetea watu waliobaguliwa na kunyanyaswa. Alichangia pakubwa juhudi za kurejeshwa kwa utawala wa vyama vingi mapema miaka ya 1990. Aidha, alichangia kupatikana kwa Katiba ya sasa, inayosheheni mapendekezo ya kulinda haki za kibinadamu na kupanuliwa mawanda ya uhuru,” shirika hilo lilisema kwenye taarifa.

“Amnesty International inampa heshima Raila Odinga si tu kama kiongozi wa kisiasa bali kama mtetezi wa haki za kibinadamu aliyejitolea kutetea haki za kijamii nchini Kenya. Kumbukumbu yake itadumu na imenufaisha mamilioni ya Wakenya,” shirika hilo linaongeza kwenye risala zake za kuomboleza Bw Odinga.

Katiba ya sasa iliyozinduliwa mnamo Agosti 27, 2010, imesifiwa kama bora zaidi duniani kwa sababu inasheheni vipengele vya kulinda haki za kibinadmu.

Katiba hiyo pia ilianzisha utawala wa ugatuzi kwa kubuni serikali 47 za kuanti kuendeleza utekelezaji wa mfumo huo.

Bw Odinga alihudumu kama Waziri Mkuu kati ya miaka ya 2008 na 2013 ambapo aliongoza shughuli za kuleta uponyaji nchini kufuatia ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka wa 2007.