Habari za Kitaifa

Raila asema ataongoza maandamano ya Saba Saba Kamukunji

Na CHARLES WASONGA July 7th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

SERIKALI imesema kuwa Julai 7, siku ya mapumziko huku taharuki ikitanda nchini Wakenya wasijue ikiwa waendelee na shughuli zao za kawaida au wabaki nyumbani.

Waziri wa Utumishi wa Umma Geoffrey Ruku jana aliwataka watumishi wa umma kufika kazini, maandamano ya kuadhimisha siku ya Saba Saba yakitarajiwa kufanyika kote nchini.

Huku akiahidi kutembelea afisi mbalimbali za serikali, Waziri alionya kuwa wafanykazi watakaosusia kazi wataadhibiwa kwa mujibu wa Sheria na Kanuni za Utumishi wa Umma.

Hata hivyo, Waziri mwenzake wa Elimu Julius Migos Ogamba na Kaimu Afisa Mtendaji wa Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC), Evaleen Mitei, hawajatoa onyo kama hilo kwa walimu hata baada ya shule kadhaa za umma kuwataka wanafunzi wasalie nyumbani leo.

“Jumatatu si siku ya mapumziko; wafanyakazi wote wa serikali sharti wafike kazini bila kuchelewa,” akasema Waziri Ruku kwenye ibada ya Jumapili Embu.

Naye Rais William Ruto, aliyehudhuria ibada hiyo, alilaani pepo wa maafa na uharibifu wa mali na kuwahimiza Wakenya kudumisha amani leo na siku zijazo.

“Ninaomba ninyi kama viongozi wa kidini mtuongoze kwa maombi ili maafa na uharibifu wa mali usishuhudiwe nchini kesho au siku nyingine. Pepo hili lituondokee kabisa ili wananchi waendelee na shughuli zao katika mazingira ya amani na utulivu,” akaeleza.

Kwa upande wake, Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen alihimiza amani huku akitoa wito kwa polisi kuzingatia utaalamu wanapokabiliana na wale watakaodiriki kujihusisha na vitendo vya uhalifu. Kinyume na wiki jana ambapo alionekana kuhimiza polisi kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya wazua vurugu, Waziri alisema polisi watakabiliana na wahalifu “kwa mujibu wa sheria”.

“Ningependa kuwahakikishia Wakenya kuwa nchi yetu, wizara yetu na serikali inayo nia nzuri ya kuhakikisha kuwa raia wanafurahia amani. Hatuna nia ya kumdhuru yeyote. Nia yetu ni kuhakikisha kuwa nchi inasalia salama,” Murkomen akaeleza akiwa Meru.

Lakini Rais Ruto na Waziri Murkomen wakiwahakikishia raia usalama, genge la wahuni jana lilivamia akina mama waliokongamana katika afisi za Tume ya Kutetea Haki za Bibinadamu Kenya (KHRC) jijini Nairobi kupanga jinsi watakavyoshiriki maadhimisho ya Saba Saba.

Naye kiongozi wa ODM Raila Odinga alitangaza kuwa ataongoza makala ya 35 ya maadhimisho hayo katika uwanja wa kihistoria wa Kamukunji, Nairobi.

Kwenye taarifa, mwanasiasa huyo mkongwe, ambaye ni mmoja wa waliokamatwa wakati wa Saba Saba ya kwanza mnamo Julai 9, 1990, aliwataka wananchi kujitokeza uwanjani humo kwa wingi kwa maadhimisho ya shinikizo hizo za kupigania demokrasia ya vyama vingi na utawala bora.

Bw Odinga alisema taifa hili bado linazongwa na masuala yale yale yaliyochochea maasi ya Saba Saba, miaka 35 iliyopita, kama vile kupanda kwa gharama ya maisha na kuhujumiwa kwa haki za kimsingi za binadamu.

“Hatujapata yale tuliitisha wakati wa maandamano ya kwanza ya Saba Saba,” akasema.

“Ukiukaji wa haki za binadamu ungali changamoto kuu, ukatili wa polisi ungalipo na hali ya uchumi haijaimarika kwani gharama ya maisha iko juu, umaskini umekithiri na vijana wengi hawana ajira. Saba Saba ililenga kuwaleta watu pamoja kwa ajili ya lengo kuu la kabadilisha hali kama hii,” Bw Odinga, ambaye ni mshirika wa Rais Ruto katika serikali jumuishi, akaeleza.

Waziri huyo mkuu wa zamani aliweka wazi kwamba anaunga mkono kampeni zinazoendeshwa na vijana wa kizazi cha Gen Z, kupigania utawala bora na kuishinikiza serikali kuheshimu haki za kimsingi za raia.

Kuhusu afisi za KHRC, wanawake watetezi wa mageuzi hayo walishambuliwa na kuporwa mali zao na kundi la wanaume walioonekana kukodiwa.

Walioshuhudia tukio hilo walisema, kundi la wanaume wapatao 10 waliwavamia mwendo wa saa saba mchana huku wakiwarushia akina mama hao matusi, wakipiga mateke viti na kuwapokonya simu, tarakilishi na mali nyinginezo.

Akina mama hao walitaka kuwahutubia wanahabari kuhusu mipango yao ya Saba Saba. Baadhi yao waliofika wakiwa wamewabeba watoto wao, walisalia hoi machozi yakiwatoka.

“Inasikitisha kuwa katika enzi kama hizi, wanawake wanazuiwa kujieleza. Nilikuja hapa na mtoto wangu na hivyo nisingetoka. Waliiba simu yangu na kuniamuru niondoke mahala hapa,” Mama Noosim Naimasiah, aliyekuja na watoto wake wawili, akasema.

Wahuni hao waliofunika nyuso zao na waliojihami kwa marungu waliwalemea walinzi wa kibinafsi na kuingia katika uwanja wa KHRC.

Baadhi ya wanawake, wanaotoka Kayole, Kibra, Kawangware na Dagoretti, waliweza kuwatambua baadhi ya wanaume hao.

Walisema kuwa wahuni hao walikodiwa kutoka mitaa ya Kibra na Dagoretti.

Licha ya kushambuliwa na kutisha, wanawake hao waliapa kuendelea kuishinikiza serikali ikomeshe kuwadhulumu raia nyakati za maandamano.

Waliapa kuungana na Wakenya wengine katika maadhimisho ya maasi ya Saba Saba.

“Kama akina mama hatuwezi kunyamaza watoto wetu wanapouawa na polisi. Maisha yana thamani kubwa. Hamna aliye na ruhusa ya kuua binadamu,” wakasema.

Akina mama hao waliwataka viongozi wa kisiasa kupigania haki za wahasiriwa badala ya kuunga mkono mswada wa kisheria unaolenga kuhujumu uhuru wa raia kujieleza na kuandamana kwa amani.

“Inavunja moyo kuona wanawake viongozi wakikimya au wakiunga mkono sheria za dhalimu zinazotuzuia kujieleza,” wakaongeza huku wakiitaka kutengwe maeeneo maalum ya wanawake kuandamana.