Raila ni ndumakuwili, aliuza wabunge kwa Ruto na sasa anawakosoa, asema Wamalwa
KIONGOZI wa chama cha Democratic Action Party of Kenya (DAP-K) Eugene Wamalwa amemponda Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga kwa kuwashutumu wabunge akidai wanahujumu utendakazi wa magavana.
Kwenye ujumbe kupitia akaunti ya X ya chama hicho, Bw Wamalwa amemtaja Odinga kama ndumakuwili asiyeweza kuaminika.
Waziri huyo wa zamani wa Ulinzi alisema Bw Odinga hawezi kuaminika anapobainisha majukumu ya wabunge kwa kuwa “amewauza wabunge wa ODM kwa Serikali,” na hivyo kuhujumu uhuru wa asasi ya bunge.
“Bw Odinga anazungumza kuhusu uhuru wa bunge na haja ya wao kufuatilia utendakazi wa serikali na kutohujumu ugatuzi, anasahau kuwa alipeana kiongozi wa wachache na maafisa wa ODM kwa serikali kuu. Huu unafiki mkubwa,” Bw Wamalwa akaeleza.
Kiongozi huyo wa DAP-K alimsuta kiongozi huyo wa ODM kwa kuendesha siasa za usaliti pale alipoagiza wabunge wa chama chake kushirikiana na utawala dhalimu wa Rais William Ruto.
Shambulio la Bw Wamalwa lilijiri baada ya Bw Odinga kuwashtumu wabunge kwa kila alichotaja ni kuhujumu ugatuzi kwa kupendekeza kupunguzwa kwa mgao wa fedha kwa serikali za kaunti kutoka Sh400 bilioni hadi Sh380 bilioni.
Kwenye kikao na wanahabari katika afisi zake zilizoko jumba la Capitol Hill, Nairobi, Bw Odinga pia aliwakashifu wabunge kwa kutwaa usimamizi wa fedha za ada ya kufadhili ukarabati wa barabara (RML) ilhali hiyo ni wajibu wa magavana.