HABARI ZA HIVI PUNDE: Raila Odinga amefariki dunia akiwa India
WAZIRI Mkuu wa zamani wa Kenya Raila Odinga alifariki dunia Jumatano asubuhi huko Koothattukulam, wilayani Ernakulam nchini India, baada ya kupata mshtuko wa moyo wakati anafanya matembezi yake ya kila asubuhi, kulingana na polisi na viongozi wa hospitali.
Odinga, mwenye umri wa miaka 80, aliangua wakati wa matembezi ya asubuhi ndani ya uwanja wa kituo cha tiba ya Ayurveda, na alikimbizwa Hospitali ya Macho ya Sreedhareeyam Ayurvedic na Kituo cha Utafiti huko Koothattukulam, ambapo alitangazwa kuwa amefariki dunia, msemaji wa hospitali hiyo alisema.
Odinga alikuwa amewasili Koothattukulam siku sita zilizopita, akiambatana na binti yake na wanafamilia wa karibu. Alikuwa akifuata mpangilio wa matembezi ya asubuhi na vikao vya matibabu hospitalini.
Mwili wake umehifadhiwa kwa sasa katika Hospitali ya Deva Matha hapa, polisi walisema.
Msemaji huyo alisema kuwa Odinga na familia yake walikuwa wakitembelea hospitali hiyo, ambayo awali ilikuwa imemsaidia binti yake kupata tena uwezo wa kuona.
Afisa wa polisi alisema kuwa taarifa kuhusu kifo cha Odinga ziliwasilishwa kwa Ofisi ya Kanda ya Usajili wa Wageni (FRRO) kwa taratibu mwafaka za sheria.
Kifo chake kimejiri siku chache baada ya kaka yake, Dkt Oburu Oginga, kuthibitisha kuwa ndugu yake mdogo, Odinga, alikuwa mgonjwa kwa muda, lakini alikuwa akindelea kupata nafuu nchini India.
Kauli yake ilijiri siku chache baada ya uvumi na taarifa zinazokinzana kusambaa kuhusu hali ya kiafya ya Kiongozi wa chama cha ODM.
Akizungumza na wanahabari wiki jana akiwa Ugunja na pia kwenye kipindi cha asubuhi katika redio ya lugha ya mama, Radio Nam Lolwe, Dkt Oginga alieleza kuwa ugonjwa huo haukuwa wa kutishia maisha.
“Raila, kama binadamu yeyote, alipata matatizo madogo ya kiafya siku chache zilizopita, lakini kwa sasa anaendelea vizuri. Alisafiri kwenda India kwa uchunguzi wa kiafya na sasa anapumzika,” alisema Dkt Oginga, ambaye pia ni msemaji wa familia ya Odinga.
Hata hivyo, kauli yake inakinzana na ile ya mke wa Raila, Mama Ida Odinga, ambaye hivi majuzi alikanusha madai kuwa mumewe ni mgonjwa, akieleza kuwa alichukua likizo fupi kutoka siasa.
“Kama mtu ninayeishi naye kila siku, naifahamu afya yake vyema kuliko mtu mwingine yeyote. Haieleweki ni vipi mtu asiyeishi naye anaweza kudai anajua hali yake ya afya kuliko mimi. Ninachowaambia ndicho ukweli,” alisema Mama Ida.
Aidha, msemaji wa Raila, Dennis Onyango, na timu yake walikuwa tayari wamekanusha madai hayo, wakisema ni propaganda za kisiasa zilizoenezwa na wapinzani.
Ingawa Bw Odinga kwa kawaida huwa wazi kuhusu hali yake ya afya, Dkt Oginga alisema kuwa lazima Raila aarifu umma kila mara kuhusu hali yake kwa kuwa yeye si rais.
“Raila si rais ambaye afya yake lazima ijulikane hadharani kila mara, hata kwa matatizo madogo kama haya. Hatukukusudia kuzungumzia suala hili hadharani, lakini kutokana na uvumi uliokuwa umeenea, tuliamua kutoa ufafanuzi,” alisema Dkt Oginga.