Habari za Kitaifa

Raila sasa aitishwa CV kabla ya kuruhusiwa rasmi kugombea kiti AUC

May 13th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA JUSTUS OCHIENG

KINARA wa upinzani Raila Odinga sasa anakodolewa macho na masharti magumu kwenye azma yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika (AUC).

Kigogo huyo wa siasa za upinzani anatarajiwa kuwasilisha stakabadhi za kuwania wadhifa huo kufikia mwisho wa mwezi huu kwa mujibu wa balozi wa zamani wa Kenya nchini Marekani Elkanah Odembo.

AU imeweka makataa ya Agosti 6 kwa wawaniaji wa wadhifa huo kuwasilisha stakabadhi zao kwa lugha mbili rasmi.

Wote wanastahili kuwasilisha wasifukazi na maelezo machache kuhusu maono yao kwa bara hili na jinsi wakatakavyokabiliana na changamoto mbalimbali zinazokumba Afrika.

“Hata hivyo, wanachama kutoka ukanda wa Mashariki wanaombwa kuwasilisha wasifukazi wao pamoja na stakabadhi hitajika kwa lugha sita tofauti,” ikasema barua ya AU.

Hii ina maana kuwa Bw Odinga pamoja na wawaniaji wengine wanaomezea mate uenyekiti wa AUC ambao umetengewa wadhifa huo, lazima waifuate amri hiyo.

Lugha hizo ni Kiingereza, Kiarabu, Kifaransa, Kireno, Kihispania na Kiswahili.

Bw Odinga anakabiliwa na upinzani kutoka kwa waziri wa zamani wa masuala ya kigeni Somalia Fawzia Yusuf na waziri wa masuala ya nje wa Djibouti Mahmoud Youssouf.

“Ana zaidi ya miaka 20 ya uzoefu kama waziri wa kigeni na pia anazungumza  Kizungu, Kifaransa na Kiarabu kwa ufasaha. Ndiye anatosha kwa wadhifa huu,” ikasema taarifa ya serikali ya Djibouti ikimpigia upato Youssouf mwezi uliopita.

Bw Youssouf amekuwa waziri wa nchi za kigeni wa Djibouti tangu 2005.

AUC pia imeweka  masharti magumu ya kiakademia ambayo kila mwaniaji anatakiwa  atimize. Kati ya hayo ni kuwa na shahada ya uzamili katika masuala ya kisheria, uhusiano wa kimataifa, upatanishi, usimamizi na kiuchumi.

Pia anahitajika awe na shahada ya uzamifu katika sayansi ya siasa, usimamizi, biashara, sheria, sayansi ya kijamii.

“Hata hivyo, si lazima mwaniaji ayatimize yote wala hayanuii kumweka katika mkataba au kandarasi ya ajira. Masharti haya yanaweza kubadilishwa na msimamizi akitekeleza majukumu yake,” ikasema AU
Taarifa hiyo inaonekana kama afueni kwa Bw Odinga ambaye serikali  imekuwa ikimvumisha achukue nafasi hiyo kutoka kwa Moussa Faki mnamo Februari mwakani.

Aidha wawaniaji pia bado hawatakuwa na mteremko kwani wanahitajika kuwa wameonyesha uongozi mzuri usiotiwa doa la ufisadi katika mashirika mbalimbali ya kitaifa na kimataifa waliyowahi kusimamia.

Katika mashirika hayo waliyosimamia, lazima waonyeshe kuwa kulikuwa na matumizi ya kuridhisha ya fedha na hakukuwa na sakata zozote zilizowasawiri vibaya.

“Lazima waonyeshe uongozi wa hekima na uwezo wa kutoa mawazo mapya na mapendekezo yatakayosaidia bara hili kuwa na amani na kupiga hatua kimaendeleo,”

Jana, serikali ilishikilia kuwa haijamtelekeza Bw Odinga na bado itakuwa ikimpigia upato apate wadhifa huo.

Hii ni licha ya kuwa kiongozi huyo wa ODM amekuwa akishiriki mikwaruzano na serikali kuhusu masuala mbalimbali ya uongozi nchini.

“Msimamo wa serikali kuhusu mwaniaji wake wa wadhifa wa AUC haujabadilika na unasalia ule ule,” Katibu wa Masuala ya Kigeni Dkt  Korir Sing’oei akasema.