• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Rais aagiza waliotoa leseni tata kituo cha gesi wafutwe kazi

Rais aagiza waliotoa leseni tata kituo cha gesi wafutwe kazi

NA WANDERI KAMAU

RAIS William Ruto ameagiza kufutwa kazi kwa maafisa wa serikali wanaolaumiwa kutoa leseni kwa kituo cha kuuzia gesi ambapo kulitokea mlipuko mkubwa katika eneo la Embakasi, Nairobi, mnamo Alhamisi usiku.

Kwenye kisa hicho, watu watatu walithibitishwa kufariki huku wengine zaidi ya 280 wakipata majeraha mabaya.

Akirejelea kisa hicho katika eneo la Lugari, Kaunti ya Kakamega, Jumamosi asubuhi, Rais Ruto alikihusisha na uwepo wa ufisadi, kutowajibika na tamaa miongoni mwa maafisa wa serikali waliotoa leseni kwa mmiliki wa kituo hicho.

Kutokana na hayo, aliiagiza Wizara ya Kawi kuhakikisha kuwa watu waliohusika kwenye utoaji leseni hiyo wamefutwa kazi mara moja na kufunguliwa mashtaka kwa makosa ya kutowajibika.

Alieleza wasiwasi wake kuwa watu walio serikalini walitoa leseni kwa kituo hicho kuendeshwa katika eneo la makazi ya watu, hivyo kuhatarisha maisha yao.

“Ningetaka kusema wazi kuwa, maafisa wa serikali walitoa leseni kwa kituo cha gesi kuendeshwa katika eneo la makazi ya watu, licha ya kufahamu walikuwa wakifanya vibaya. Walifanya hivyo kutokana na ufisadi na kutowajibika.

Leo, kuna watu waliojeruhiwa. Tuna Wakenya waliofariki. Lazima Wizara iwachukulie hatua, kwa kuhakikisha kuwa wamefutwa na kufunguliwa mashtaka kwa makosa waliyofanya,” akasema Rais.

Alisema kuwa hakuna haja yoyote watu kama hao kuendelea kuhudumu serikalini na kulipwa mishahara kwa pesa za walipaushuru.

Mnamo Ijumaa jioni, serikali ilitangaza mipango ya kuanza msako mkali dhidi ya vituo vya kuhifadhi na kujaza gesi kote nchini kutokana na kisa hicho.

Kwenye taarifa ya pamoja, Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na mwenzake Davis Chirchir (Kawi), walisema kuwa serikali itabomoa vituo vyote ambavyo havijazingatia kanuni zilizoweka.

Hata hivyo, Muungano wa Vyama vya Wakazi Kenya (KARA) umeilaumu serikali kwa kulegea kwenye juhudi za kuhakikisha inawalinda raia dhidi ya hatari kama hizo.

  • Tags

You can share this post!

Embakasi: Nema yatimua maafisa wanne kwa kutoa leseni tata

Nigeria pazuri kuzoa taji la nne la Afcon baada ya kudengua...

T L