Rais alivyojitokeza bila mlinzi akitimua mawaziri
KINYUME na ilivyo desturi yake wakati akihutubia taifa, Rais William Ruto Alhamisi, Julai 11, 2024 wakati akivunja Baraza la Mawaziri hakuwa ameandamana na mlinzi wake.
Kwenye hotuba yake iliyochukua dakika chache tu, Rais Ruto alisimama kidete mbele ya maikrofoni za vyombo vya habari akiwa peke yake na kuporomosha tangazo ambalo limeandaa jukwaa la mazungumzo mazitio kote nchini.
Mlinzi wake wa karibu, hakuwepo.
Kiongozi wa taifa pia hakuwa ameandamana na naibu wake, Bw Rigathi Gachagua, Mkuu wa Maziri, Bw Musalia Mudavadi na viongozi wengine wa hadhi ya juu serikalini.
Isitoshe, mazingira ya jukwaa alilohutubia katika Ikulu, Nairobi, hayakuwa na yeyote.
Wanahabari kutoka mashirika mbalimbali ya habari yaliyopeperusha hotuba ya Dkt Ruto mbashara ndiyo walikuwa, japo hawakupewa fursa ya kurusha maswali.
Hata ingawa alitetea serikali yake ya Kenya Kwanza katika kile alihoji kama kusaidia kuboresha gharama ya maisha, hatua ya kuvunja Baraza la Mawaziri imechochewa kwa kiasi kikubwa na maandamano ya vijana barobaro, Gen Z.
Vijana hao wamekuwa wakishiriki maandamano ya kitaifa kushinikiza serikali kushusha gharama ya maisha, ikiwemo kupunguza ushuru, kuwaandalia jukwaa mahususi la kupata kazi na mazingira bora ya ajira na biashara.