Rais atia saini Mswada wa Matumizi ya Fedha za bajeti ili operesheni za serikali ziendelee
RAIS William Ruto ametia saini Mswada wa Matumizi ya Fedha za Bajeti ya 2024 ili kuendeleza operesheni za serikali.
Haya yanajiri baada ya mikakati ya serikali ya kulazimisha kupitishwa kwa Mswada wa Fedha wa 2024 kugonga mwamba.
Kwa kawaida, Mswada wa Fedha huandamana na Mswada wa Matumizi ya Fedha ambao unaipa Serikali mamlaka ya kisheria kukusanya mapato kupitia mapendekezo yaliyonakiliwa kwenye Mswada wa Fedha.
Rais pia ameelekeza Hazina ya Kitaifa kuandaa makadirio ya bajeti ili kupunguza gharama kwa kiwango ambacho kilitarajiwa kuongezeka kupitia Mswada wa Fedha 2024 uliotupiliwa mbali, kwa sababu sasa taifa litaendelea na Bajeti ya 2023 hadi mswada mwingine wa fedha wa 2024 utengenezwe.
“Mzigo wa kupunguzwa kwa matumizi ya kima cha Sh346 bilioni utagawanywa sawia na ngazi zote za serikali: serikali ya kitaifa na zile za kaunti,” alisema Rais.
“Kuhusiana na matumizi ya Serikali ya Kitaifa, kupunguzwa kwa mgao kutaathiri baraza la mawaziri, mabunge, idara ya mahakama, na tume za kikatiba.”
Kiongozi wa taifa anayekabiliwa na pingamizi kali kutoka kwa vijana wa kizazi cha Gen Z alieleza kuwa katiba inamhitaji kusaini mswada wa matumizi ya fedha kabla ya Juni 30 kila mwaka ili mipango ya serikali isikwame.
“Vifungu vya 221 na 222 vya katiba vinahitaji mswada wa matumizi ya fedha uwe sheria kuhakikisha shughuli za serikali zinaendelea, hasaa utoaji wa huduma muhimu,” alieleza Rais.
Kuenda sambamba na kuanguka kwa Mswada wa Fedha wa 2024, Dkt Ruto amerejesha katika Bunge la Kitaifa Mswada wa Mgao wa Kaunti na ule wa Mapato ili makadirio yapunguzwe.
Isitoshe, Hazina ya Kitaifa imeelekezwa kuwasilisha marekebisho kwa Sheria ya Ugavi wa Mapato ya 2024 ili iakisi athari ya hatima ya Mswada wa Fedha wa 2024.
Kulingana na amri ya Rais, ni jukumu la Wizara ya Fedha kuhakikisha maafisa wa uhasibu wanakuwa chonjo kudhibiti ufadhili wa huduma muhimu usitumie zaidi ya asilimia 15 ya bajeti hadi bajeti ya ziada iidhinishwe.