• Nairobi
  • Last Updated April 12th, 2024 5:55 PM
Rais Ruto apokea mwaliko rasmi kumtembelea Joe Biden

Rais Ruto apokea mwaliko rasmi kumtembelea Joe Biden

NDUBI MOTURI Na HASSAN WANZALA

RAIS William Ruto na Mama wa Taifa Rachel Ruto wamepokea mwaliko kwa ziara rasmi nchini Marekani mnamo Mei 23, 2024, ambapo mwenyeji wao, Rais Joe Biden ataongoza maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano kati ya Marekani na Kenya.

Ikulu ya White House, kupitia kwa katibu wa kitengo cha habari Karine Jean-Pierre, amesema ziara hiyo itaimarisha uhusiano kati ya mataifa hayo.

“Aidha, kwenye ziara hiyo, viongozi wa mataifa haya mawili wataangazia amani na usalama, namna ya kupanua ushirikiano wa kiuchumi, na kuimarisha misingi ya demokrasia,” amesema Bi Jean-Pierre.

Rais Ruto kwa upande wake amepokea mwaliko huo kwa furaha, akisema Kenya na Marekani zitaimarisha ushirikiano wa kunufaisha raia wa mataifa hayo.

“Ziara hiyo itasaidia kuangazia masuala ya biashara na uwekezaji, nishati safi na uhifadhi wa mazingira, teknolojia ya masuala ya kidijitali na uvumbuzi, afya na maendeleo ya binadamu, amani na usalama pamoja na ushirikiano wa maendeleo ya kudumu yanayofaidi Kenya, Afrika, mataifa yanayoendelea na dunia kwa ujumla,” akachapisha Rais Ruto kwenye mtandao wa X (zamani Twitter).

Vilevile yaliyopitishwa wakati wa kongamano kuu la Marekani na viongozi wa Afrika mnamo Desemba 2022 yatakuwa miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa.

Hii ndio itakayokuwa ziara rasmi ya Rais Ruto kumtembelea Rais wa Marekani.

Mnamo Septemba 2023 Rais Ruto alihudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa (UNGA).

Pia alizuru Silicon Valley kutafuta ushirikiano na kampuni za teknolojia.

Pia mnamo Septemba 2022 alihudhuria mkutano wa UNGA akiwa Rais ‘mbichi’ kabisa baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9, 2022.

  • Tags

You can share this post!

Wazee walaani mazoea ya viongozi Kisii kurushiana cheche...

Familia ya Kiptum kujengewa nyumba aushi kwa amri ya Ruto

T L