Habari za Kitaifa

Rais Ruto kufanya ziara ya siku tatu Bungoma

May 29th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA JESSE CHENGE

RAIS William Ruto anatarajiwa kufanya ziara ya siku tatu katika Kaunti ya Bungoma, ambayo itahusisha sherehe za 61 za Madaraka Dei.

Wakazi wa kaunti hiyo wana matarajio makubwa kutoka kwa Rais Ruto, ikiwa ni pamoja na kutatua masuala kuhusu malipo ya wakulima na wafanyakazi wa kiwanda cha sukari cha Nzoia.

“Ninaamini ziara ya Rais Ruto itatusaidia kutatua changamoto zetu za maendeleo, hasa masuala kama malipo kwa wakulima wa miwa na wafanyakazi wa kiwanda cha Nzoia,” alisema Bw Bernard Makaazi, ambaye ni mkazi wa Bungoma.

Pia wanatarajia ujenzi wa barabara ya Musikoma-Buyofu, usambazaji wa umeme mashinani, na kuimarishwa kwa barabara ya Chwele-Lwakhakha, pamoja na miradi mingine ya maendeleo.

“Ni faraja kubwa kuona Rais Ruto akichukua muda wa kututembelea. Tunatumai atapata suluhu kwa changamoto zetu zinazohusu hitaji la maendeleo,” alisema Bi Nancy Jumba.

Dkt Ruto katika ziara yake atafungua miradi mbalimbali kuanzia Uwanja wa Masinde Muliro ulioko Kanduyi, Kituo cha Uhamiaji na Pasipoti, na Ikulu Ndogo ya Bungoma.

Uwanja wa Masinde Muliro Kanduyi utakaotumika kwa sherehe za Madaraka Dei mnamo Juni 1, 2024. PICHA | JESSE CHENGE

Aidha, kiongozi wan chi atakagua uwanja mdogo wa ndege wa Matulo, kituo cha mawasiliano na teknolojia, na utandawazi, miongoni mwa miradi mingine inayolenga kuinua maendeleo ya Kaunti ya Bungoma.

“Tunamkaribisha Rais Ruto kuja kuzuru eneo letu. Ni jambo la heri ikizingatiwa Bungoma ulikuwa mji ambao ulisahaulika kwa kiasi kikubwa, lakini sasa huduma za serikali zinaimarika,” akasema Bw Siele Danson.

Hii itakuwa mara ya tatu kwa Rais Ruto kuzuru Kaunti ya Bungoma tangu achukue hatamu za uongozi mnamo Septemba 13, 2022.

Wananchi wana shauku kubwa, wakisubiri ziara yake kwa hamu kubwa na matumaini ya maboresho ya hali yao ya maisha.

Kauli mbiu ya maonyesho yanayotarajiwa kufanyika Bungoma ni “Kilimo Biashara” ambapo lengo ni kuonyesha juhudi za serikali katika kuendeleza sekta ya kilimo kuwa tegemeo la uchumi wa taifa. Ujio wa Rais Ruto unatarajiwa kuleta nuru na matumaini kwa wakazi wa Bungoma.

Siku ya Madaraka Dei, Kaunti ya Bungoma inatarajiwa kuwa mwenyeji wa wageni mbalimbali kutoka tabaka tofauti, akiwemo Rais Ruto.

Uwanja wa Masinde Muliro Kanduyi utakaotumika kwa sherehe za Madaraka Dei mnamo Juni 1, 2024. PICHA | JESSE CHENGE

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Bungoma Bw Francis Kooli alisema usalama umeimarishwa hata zaidi ikilinganishwa na hali ya kawaida huku vitengo vyote vya usalama vikiwakilishwa.

“Tunavyo vitengo vyote vya usalama hapa, ikiwa ni pamoja na kitengo cha majibwa, farasi, maji, angani na vingine vingi. Usalama utaimarishwa kabla, wakati na baada ya sherehe hizo,” alisema Bw Kooli.

Aliongeza kwamba malori ya masafa marefu yatasitisha uchukuzi katika barabara ya Webuye-Malaba siku hiyo ya Madaraka.

Walishawasilisha ombi rasmi kwa Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama Barabarani (NTSA).

[email protected]