Rais wa zamani Ghana alivyotumia suala la uchumi kuporomoka kurejea mamlakani kama Trump
ACCRA, Ghana
ALIYEKUWA Rais wa Ghana John Dramani Mahama amerejea mamlakani baada ya kushinda katika uchaguzi wa urais uliofanyika nchini humo Jumamosi.
Hii ni baada ya mpinzani wake mkuu Makamu Rais Mahamudu Bawumia kukubali kushindwa Jumapili, Desemba 8, 2024.
Sawa na Rais Mteule wa Amerika Donald Trump, Mahama alikita kampeni zake katika uchumi ambao umedaiwa kusambaratika chini ya uongozi wa Rais Nana Akufo Addo na makamu wake Bawumia. Taifa hilo hivi majuzi lilishindwa kulipa madeni yake, kwa mara ya kwanza tangu kujipatia uhuru.
Akiongea na wanahabari katika makazi yake, Bawumia alisema amempigia simu Mahama na kumpongeza kwa ushindi.
NDC ilishinda pia viti vingi vya ubunge
Aliongeza kuwa chama cha Bw Mahama, National Democratic Congress (NDC) pia kilishinda viti vingi vya ubunge.
“Data kutoka kwa kituo chetu cha kujumuisha kura za urais zinaonyesha kuwa aliyekuwa Rais John Dramani Mahama ameshinda katika uchaguzi wa urais na kura nyingi zaidi,” Bawumia akasema.
Dkt Bawumia alisema alikubali kushindwa kabla ya matokeo rasmi kutangazwa ili kupunguza taharuki nchini Ghana.
Kabla ya tangazo lake, vurugu ziliripotiwa katika vituo kadhaa vya kujumuisha kura katika maeneo bunge ambako matokeo yalikuwa yakipokewa kutoa vituo vya kupigia kura.
“Nitatoa taarifa hii ya kukubali kushindwa kabla ya Tume ya Uchaguzi kutangaza matokeo rasmi ili kuzima taharuki na kudumisha amani nchini mwetu,” Bawumia akasema.
“Ni muhimu kwa wawekezaji kutoka mataifa ya ng’ambo kuendelea kuwa na imani na chaguzi za Ghana ambazo huendeshwa kidemokrasia na katika mazingira ya amani,” akaongeza.
Bawumia ampongeza kwa ushindi
Kwa upande wake Mahama alikubali kuwa alipokea simu kutoka kwa Bawumia akimpongeza kwa ushindi.
“Leo asubuhi, nimepokea simu ya pongezi kutoka kwa ndugu yangu Dkt Bawumia, kufuatia ushindi wangu wa wazi katika uchaguzi wa Jumamosi. Asante Ghana kwa kurejesha imani yenu kwangu,” Mahama akasema kupitia ujumbe kwenye mtandao wa kijamii wa X.
Mahama, 66, ambaye alihudumu kama Rais wa Gahana kuanzia 2012 hadi 2016, alimtaja Bawumia kama ambaye ataendeleza sera ambazo zilichangia Ghana kutumbukia katika changamoto kubwa ya kiuchumi.
Rais wa sasa Nana Akufo-Addo amestaafu rasmi baada ya kuhudumu kwa mihula miwili inayoruhusiwa na Katiba ya sasa.