Habari za Kitaifa

Ripoti: Serikali imejaa wakuu walio na vyeti bandia

Na STEVE OTIENO May 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 3

IMEBAINIKA kuwa zaidi ya watumishi wa umma 3,000, wakiwemo maafisa wakuu wa mashirika, maafisa wakuu watendaji wa mashirika, wakuu wa polisi na hata wapelelezi wa usalama, walitumia vyeti bandia kupata ajira serikalini.

Hii ni kwa mujibu wa utafiti ambao ulifanywa na Tume ya Kuwaajiri Watumishi wa Umma Nchini (PSC) wakikagua vyeti vya masomo na vile vya kitaaluma vya maafisa wa umma.

Mkuu wa Utumishi wa Umma, Felix Koskei jana alisema vyeti feki ni hatari kwa sababu ni kikwazo katika kutimiza ajenda ya serikali.

“Vyeti feki vimekuwa vikipatikana katika kila sekta ya utumishi wa umma, serikali ya kitaifa na ya kaunti, mashirika, tume na hata afisi huru,” akasema Bw Koskei.

Alikuwa akiongea wakati wa Kongamano na Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi (EACC) lililolenga kuhakikisha uhalali wa vyeti vya masomo na vile vya kitaaluma.

Bw Koskei alifichua matokeo ya utafiti huo wa PSC, akisema kati ya vyeti vya watu 28,000 vilivyowasilishwa kwa Baraza la Mitihani ya Kitaifa kutoka taasisi 91 za umma, zaidi ya 1,280 vilikuwa vimeghushiwa na vilikuwa feki.

Pia, maafisa 787 wa umma kati ya 29,000 ambao wanafanya kazi katika wizara 195, idara na mashirika, vyuo vikuu na vile vya kiufundi, hawakuwa na vyeti halali.

Maafisa hao iligunduliwa walipata ajira, wakapandishwa ngazi na kupewa kazi nyingine za hadhi ilhali walitumia stakabadhi ghushi.

“Hii ni picha na taswira mbaya kwa wakuu wa mashirika, wenyekiti, wanachama wa bodi, polisi na wapelelezi wa usalama katika mashirika mbalimbali ambao walipatikana na vyeti ghushi.

“Hawa watapeleka nchi katika mkondo usiofaa siyo kwa sababu wanataka ila kwa sababu wana ujuzi finyu kutekeleza majukumu yao,” akaongeza.

Mkuu huyo wa utumishi wa umma alisikitika kwamba, ukora huo upo katika viwango vyote vya elimu kuanzia shule ya msingi hadi kiwango cha juu kabisa cha kuhitimu.

Kwa mujibu wa Bw Koskei, takwimu kutoka ripoti ya PSC ya 2023/24 ilifichua kuwa, taasisi 358 zilikagua vyeti vya maafisa 116,000 ambapo 859 walipatikana na vyeti feki huku vingine 24,000 vikikosa kukaguliwa kabisa.

Wale wanaoongoza katika vyeti ghushi ni mashirika ya serikali ambapo asilimia 70 za stakabadhi si halali huku ikifuatwa na vyuo vikuu kwa visa 116.

Hata hivyo, taasisi 49 pekee ziliwasilisha majina ya maafisa walioghushi vyeo kwa EACC na PSC ilhali taasisi 43 hazikutoa ushahidi kuwa zilifanya hivyo.

Kati ya 49, taasisi nne ziliwasilisha orodha ya maafisa waliokuwa na vyeti ghushi hali ambayo ilikuwa tofauti na ile iliyothibitishwa na mashirika yao.

“Hali hii inatuweka pabaya kwa sababu watu ambao Wakenya wanatarajia wawahudumie ni wale ambao hawana ujuzi, wamefeli na bado wanaendelea kuwa afisini,” akasema.

Bw Anthony Muchiri kutoka PSC alisema kuandaliwa kwa kongamano kuhusu matumizi ya stakabadhi ghushi kupata ajira ni ishara kwamba, hali ni mbaya katika sekta zote nchini.

Alitoa mfano wa wasomi ambao wanafika kwenye mahojiano wakiwa na vyeti vya uzamili na uzamifu, ilhali baadhi yao hawawezi kujieleza na ni vigumu kubaini iwapo wamefuzu kihalali.

“Kile ambacho hutoka kwa midomo yao ni tofauti. Wengine ukiona stakabadhi zao, ndiyo ni halali, lakini kinachotokea kwa midomo yao kinaonyesha kuwa akili yao si sawa na walizipata bila masomo ya kiwango hicho,” akasema Bw Muchiri.

Aliongeza kuwa mnamo Februari 2024, PSC ilianza mchakato wa kuhakiki vyeti 53,000 vilivyowasilishwa kwa watumishi wa umma kati ya 2012 na 2022.

“Kati ya 53,000 zaidi ya 2,500 au 3,000 zilikuwa ghushi. Hapa hujajumuisha vyeti halali ambavyo vilipatikana kwa njia ya ukora na sasa vyeti vyote vya watumishi wa umma kutoka shule ya msingi, sekondari hadi vile vya uzamifu lazima vihakikiwe na kukaguliwa,” akaongeza Bw Muchiri.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mtendaji wa EACC Abdi Mohamud alisema kuwa tangu 2022, tume hiyo imechunguza visa 549 vya vyeti vilivyoghushiwa.

“Kati ya hizi, faili 134 zimekamilishwa huku 85 zikiwasilishwa kwa afisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma na 33 bado ziko kortini. Zaidi ya kesi 20 zimekamilishwa na 13 wakahukumiwa huku saba wakiondolewa kesi,” akasema.

Bw Mohamed alifichua kuwa, EACC inapanga kutwaa zaidi ya Sh460 milioni ambazo watumishi wa umma waliopata ajira kwa kutumia vyeti feki, walilipwa.

Mwenyekiti wa EACC, Askofu David Oginde naye alisema ajira kwa kutumia vyeti feki katika utumishi wa umma ni dondasugu ambalo limeenea kwenye sekta zote.

Alifichua kuwa amekuwa akikemewa aliposema atakuwa akiendea mali ya waliotumia vyeti feki kupata ajira na kulipwa mishahara, wengi wakisema wanaondamwa walitumia nguvu zao kuwawajibikia Wakenya.

“Ndiyo walitoa huduma lakini huduma zenyewe zilikuwa duni na hazikufika ubora unaohitajika,” akasema.

Askofu huyo aliongeza kuwa, sekta ya kibinafsi haijaachwa nyuma kwa kuwa baadhi ya walioajiriwa huko wanatumia stakabadhi ghushi na wanatoa huduma ambazo hawajafuzu kuzitoa.

Afisa huyo alisikitika kuwa Kenya inaelekea kupoteza hadhi yake kama inayotoa wanataaluma ambao wamefuzu na wanatoa huduma bora iwapo ukora wa kupata vyeti ghushi bado utaendelea.