Habari za Kitaifa

Ripoti yafichua jinsi magenge yamejaa nchini

Na STEVE OTIENO December 3rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI imefichua kukithiri kwa magenge ya wahalifu nchini na wanakopatikana, ikionyesha jinsi baadhi ya makundi haya yanavyohusika na vurugu za kisiasa, kunyanyasa wananchi, wizi wa ardhi, ulaghai na kudhulumu jamii.

Haya yamefichuliwa katika ripoti ya Jukwaa la Usalama, iliyotolewa na Rais William Ruto katika Ikulu jijini Nairobi, na kuanika wazi zaidi tatizo ambalo limekuwa likidumu kwa muda mrefu bila kutajwa.

Ripoti inaonyesha uwepo wa mamia ya magenge Nairobi, Pwani hadi Rift Valley. Nairobi pekee ina zaidi ya magenge 130, ikiwa ni pamoja na kufufuliwa kwa Mungiki, moja ya makundi maarufu ya uhalifu nchini.

Makundi haya huzua vurugu za kisiasa, utekaji nyara, ukandamizaji wa wapiga kura na wizi, huku mara nyingi wakijitokeza wakati wa uchaguzi kwa maslahi ya kisiasa.

Katika kaunti za Magharibi, kama Kakamega, Bungoma, Busia na Trans Nzoia, makundi kama Jeshi Jinga, 42 Brothers, M23, Kapenguria Six na Usiku Sacco huzua vurugu, kutisha wananchi, na kushirikiana na wanasiasa kudhibiti maeneo.

Vile vile, Nakuru kuna makundi kama Confirm Gang na Wateitei yanayohusika na uhalifu.

Katika eneo la Pwani, makundi kama MRC, Panga Boys, Team Mashamba na Mawoz yamehusika na wizi wa ardhi, ukandamizaji na ulaghai.

Kilifi inakabiliwa na mashambulizi kutoka Team Mashamba, Mawoz na mabaki ya Mungiki, huku Panga Boys Kwale wakiwa wamepungua lakini bado ni tishio.

Machakos na Murang’a zinakabiliwa na makundi yanayohusiana na uhalifu wa ardhi na madini, baadhi yakiwa na uhusiano wa kisiasa.

Rais Ruto alisema kuwa kipindi cha kuruhusu machifu kukabili magenge bila msaada lazima kiishe. Kuimarishwa kwa kitengo cha polisi wa utawala wa mkoa (NGAPU) kunalenga kuwa na maafisa 1,860 kusaidia machifu katika vijiji, wakiwapa ulinzi wa moja kwa moja, kuimarisha ulinzi wa jamii na kukabili magenge.

Bajeti za machifu pia zimeongezwa kwa Sh15,000 kila robo mwaka ili kuboresha ufuatiliaji, usalama na ukusanyaji wa taarifa.

Kila chifu atapewa kompyuta ndoto kuwasilisha ripoti za uhalifu, ukaguzi wa mali, dawa zs kulevya na vurugu za kijamii.

Mfumo huu utarahisisha mawasiliano na polisi na kuhakikisha hatua za haraka zinachukuliwa, hasa katika maeneo ambapo magenge hujipanga upya baada ya kukamatwa.

Ripoti pia inaangazia uhusiano kati ya matumizi ya dawa za kulevya na uajiri wa magaidi, hususan kwa vijana wasiokuwa na ajira.

Kutokana na hili, serikali imeagiza upanuzi wa kitengo cha kukabiliana na dawa za kulevya, kuanzishwa kwa ofisi 34 za kikanda, na kusimamia leseni za pombe ili kupunguza ununuzi haramu wa pombe.

Zaidi ya hayo, serikali itajenga vituo 900 vya polisi, kuanzisha wilaya ndogo ili kuweka mamlaka ya serikali karibu na wananchi.

Wazee wa vijiji watatambuliwa rasmi, kupewa kitambulisho cha serikali na kulipwa Sh 3,000 kila mwezi kama motisha kutoa taarifa za mapema.