Habari za Kitaifa

Rotich akamata mnofu serikalini baada ya korti kumsafisha

February 8th, 2024 Kusoma ni dakika: 2

NA CHARLES WASONGA

UTEUZI wa aliyekuwa Waziri wa Fedha Henry Rotich kuwa Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kifedha na Sera ya Bajeti katika Ofisi ya Rais umeongeza orodha ya wandani wa Rais William Ruto ambao wanaendelea kutunukiwa minofu baada ya kufutiwa makosa katika kesi za ufisadi.

Wengine walitunukiwa vyeo hata kabla ya kesi zao kuisha hali iliyoibua pingamizi kutoka kwa wanasheria na Wakenya kwa ujumla.

Baadhi yao ni Joe Sang aliyeteuliwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Usafirishaji Mafuta Nchini (KPC) baada ya kuondolewa kesi ya ufisadi wa kima cha Sh1.9 bilioni.

Mwingine ni mfanyabishara Mary Wambui ambaye mnamo Januari 2023 aliondolewa kesi ya ukwepaji ushuru wa Sh2.2 bilioni kisha akateuliwa kuwa Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mawasiliano Nchini (CA).

Uteuzi wa Bw Rotich Alhamisi Februari 8, 2024 unajiri mwezi mmoja na nusu baada ya kesi dhidi yake kuhusu sakata ya ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer. kusambaratika mnamo Desemba 14, 2023.

Hakimu wa Mahakama ya Eunice Nyutu alimwachiliwa huru Bw Rotich na maafisa wengine 14, kutokana na ukosefu wa ushahidi wa kutosha kuhimili kesi zilizowakabili.

Uteuzi wa Bw Rotich ulitangazwa kupitia barua iliyoandikwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei na kutumwa kwa vyombo vya habari.

“Kupitia barua hii, umma unajulishwa kwamba Mheshimwa Rais William Ruto amemteua Waziri wa zamani wa Fedha Henry Rotich kuwa Mshauri Mkuu wa Masuala ya Kifedha na Sera za Bajeti katika Afisi yake,” Bw Koskei akasema kupitia barua hiyo.

Bw Rotich aliteuliwa kama Waziri wa Fedha mnamo 2013 wakati wa utawala wa Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

Alipigwa kalamu mnamo Januari 14, 2020, baada ya kushtakiwa kwa makosa ya ukiukaji wa sheria za utoaji zabuni za umma na wizi wa pesa za umma katika mpango wa utekelezaji wa ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer.

Bw Rotich ametunukiwa mnofu saa chache baada ya Mwenyekiti wa Mamlaka ya Ukusanyaji Ushuru Nchini (KRA) Anthony Mwaura kuondolewa lawama kuhusiana na kesi ya ufisadi.

Katika uamuzi wake, Hakimu Nyuttu, (ambaye alimwachilia Rotich) alisema Jumatano kwamba hakukuwa na ushahidi wa kutosha kuhimili kesi dhidi ya Bw Mwaura na mkewe Rose Njeri na wengine walioshtakiwa kwa sakata ya ufisadi ya Sh357 milioni.

Kabla ya kuteuliwa kwake kama mwenyekiti wa KRA, Bw Mwaura alihudumu kama Mwenyekiti wa Bodi ya Kitaifa ya Uchaguzi (NEB) ya chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Wandani wengine wa Rais Ruto ambao kesi za ufisadi dhidi yao zimeporomoka tangu aingie Ikulu mnamo Septemba 13, 2022, ni Naibu Rais Rigathi Gachagua na mawaziri Mithika Linturi (Kilimo), Aisha Jumwa (Jinsia) na aliyekuwa Afisa Mkuu Mtendaji wa Kampuni ya Kenya Power Ben Chumo.