Rubani ahojiwa kuhusu mauti ya Jenerali Ogolla
RUBANI kutoka idara ya jeshi la angani ambaye aliendesha helikopta iliyomuua aliyekuwa Mkuu wa Jeshi Francis Ogolla na watu wengine tisa mwezi uliopita, ni kati ya waliohojiwa na wanaoendesha uchunguzi kuhusu kisa hicho.
Pia wanajeshi wawili wa KDF ambao walinusurika wamehojiwa huku jeshi likisema uchunguzi huo utakuwa wa kina na utachukua kipindi kirefu.
Kwenye ujumbe uliotumiwa Taifa Leo, idara ya mawasiliano ya jeshi haikufafanua maswali ambayo marubani waliowahi kuendesha ndege hiyo waliulizwa.
Ndege hiyo ilianguka baada ya kupaa angani saa nane na dakika 20 mnamo Aprili 18 katika eneo la Sindar, Kaunti ya Elgeyo-Marakwet.
“Walioshuhudia tukio hilo walihojiwa hasa waliofika wa kwanza kwenye ajali hiyo punde baada ya kutokea,” ukasema ujumbe huo.
KDF ilisema uchunguzi huo unaongozwa na Brigedia Mohamud Salah Farah kutoka kambi ya jeshi ya Laikipia.
Rais William Ruto alikuwa ametangaza kuwa Meja Jenerali John Omenda alikuwa akiongoza uchunguzi huo ila aliteuliwa Naibu Mkuu wa Majeshi na kupandishwa cheo kuwa luteni jenerali.