Habari za Kitaifa

Rudini kazi au mfutwe kazi, madaktari waonywa

March 27th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

BARAZA la Magavana (CoG) sasa linawataka madaktari wanaogoma kurejea kazini la sivyo wapigwe kalamu.

Mwenyekiti wa CoG Anne Waiguru alisema Jumatano kwamba madaktari hao wanafaa kuheshimu uamuzi wa mahakama iliyoharamisha mgomo huo ili kutoa nafasi kwa mazungumzo.

Maagizo hayo ya mahakama yalitolewa Machi 13, 2024 na Machi 15, 2024.

“Tunatoa wito kwa madaktari ambao wanagoma kurejea kazini. Wasipofanya hivyo, serikali husika za kaunti ambazo ndizo waajiri wao, zitakuwa huru kuwachukulia hatua zozote za kinidhamu,” Bi Waiguru akasema kwenye kikao na wanahabari katika makao makuu ya CoG, Westlands, Nairobi.

Bi Waiguru ambaye ni Gavana wa Kirinyaga, alitoa agizo hilo baada ya kuongoza mkutano wa mashauriano na magavana kadhaa kujadili changamoto hiyo ambayo imekwamisha huduma za matibabu katika hospitali za umma.

Aliwataka madaktari hao kutumia nafasi ambayo wamepewa na serikali ya kitaifa na zile za kaunti ili kufika katika meza ya mazungumzo kushughulikia malalamishi yao.

Bi Waiguru alisema kuwa mazungumzo yanaweza tu kufanyika kuanzia ngazi za kaunti kabla ya kufikishwa ngazi za kitaifa.

Mgomo huo uliingia siku yake ya 14 mnamo Jumatano huku viongozi wa Chama cha Madaktari Nchini (KMPDU) wakishikilia kuwa utaendelea ikiwa matakwa yao hayatatimizwa.

Madaktari wanataka msururu wa ahadi walizopewa zitimizwe, yakiwemo makubaliano ya nyongeza ya mishahara ya mwaka wa 2017.

Madaktari hao pia wanataka madaktari wanafunzi waajiriwe, wale wanaotaka kusomea shahada za juu wapewe nafasi hiyo, madaktari zaidi waajiriwe na wapewe bima ya matibabu.

Hata hivyo, Bi Waiguru alisema kuwa wajibu wa uajiri wa madaktari wanafunzi ni wa serikali ya kitaifa wala sio serikali za kaunti.