Ruth Chepngetich aibuka mwanamke wa kwanza kabisa kutimka kilomita 42 kwa chini ya saa 2:10
WAKENYA John Korir na Ruth Chepngetich wameibuka washindi wa makala ya 46 ya Chicago Marathon nchini Amerika.
Korir ametawala mbio hizo za kilomita 42 kwa saa 2:02:43 akifuatwa kwa karibu na Muethiopia Mohamed Esa (2:04:39) na Wakenya Amos Kipruto (2:04:50), Vincent Ngetich (2:05:15) na Daniel Ebenyo Simiu (2:06:04) katika usanjari huo.
Dakika chache baadaye, bingwa wa dunia mwaka 2019 Ruth Chepngetich alinyakua taji lake la tatu la Chicago Marathon kwa rekodi mpya ya dunia 2:09:57.
Chepngetich amefuta rekodi ya bingwa wa Berlin Marathon mwaka 2023 Tigst Assefa kutoka Ethiopia (2:11:53) kwa karibu dakika mbili.
Chepngetich aliyemaliza makala ya 2023 nyuma ya Mholanzi Sifan Hassan ni mwanamke wa kwanza kabisa kukamilisha 42km chini ya saa 2:10.