Ruto aahirisha ufunguzi wa shule kwa muda usiojulikana
NA MWANDISHI WETU
SERIKALI sasa imeahirisha kwa muda usiojulikana kufunguliwa kwa shule kwa Muhula wa Pili kutokana na mvua kubwa na mafuriko yanayoendelea kushuhudiwa nchini.
Akitangaza hatua hiyo Ijumaa katika Ikulu ya Nairobi, Rais William Ruto alisema kwamba ameagiza Wizara ya Elimu kusitisha mipango ya ufunguzi wa shule hadi pale utathmini wa kina utafanywa na mwongozo mpya kutolewa.
Dkt Ruto alianza hotuba kwa kuelezea jinsi janga la mvua kubwa na mafuriko limeathiri sehemu nyingi nchini huku pia Kimbunga Hidaya kikitarajiwa kugonga Pwani ya Kenya wikendi hii.
Alifafanua kwamba athari zinazoendelea kuonekana zimetokana na mabadiliko ya tabianchi na kwamba ipo haja ya washirika wa kimaendeleo kuzidisha usaidizi wa kukabiliana nazo ili kupunguza mahangaiko ya wakazi.
Kuahirishwa kufunguliwa kwa shule kumejiri wiki moja baada ya hatua kama hiyo kuchukuliwa na Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu alivyofanya Jumapili usiku wa manane.
Alikuwa amependekeza shule zifunguliwe Mei 6, 2024.
Wakati mwingine ambapo kalenda ya shule ilivurugwa ilikuwa kipindi kile cha janga la corona.