Ruto aangazia mafanikio ya utawala wake Wakenya wakilia
RAIS William Ruto Alhamisi aliendelea kutoa ahadi kwa Wakenya huku akitaja mafanikio ambayo utawala wake umeafikia kwa miaka miwili ya uongozi wake.
Rais Ruto alizungumzia hatua ambazo amepiga kwenye sekta ya afya, kilimo, kawi, fedha na uchumi wakati ambapo Wakenya nao wamekuwa wakililia changamoto mbalimbali zinazogubika nchi.
Alikuwa akizungumza bungeni kwa kikao jumuishi cha mabunge ya seneti na ya kitaifa wakati wa kutoa hotuba yake ya kila mwaka kwa asasi hizo mbili za kutunga sheria.
Katika sekta ya kilimo, Rais alisema kuwa utawala wake umetoa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima waliojisajili milioni 6.45 katika kaunti 45 kisha ikawasambazia magunia milioni saba.
“Kutokana na hilo tuna magunia milioni 47 ya kilo 90 za mahindi, maharagwe milioni 8.8, magunia milioni 10.4 na magunia milioni 2.1 ya mpunga. Polepole tutahakikisha kuwa Kenya inajitosheleza kwa chakula,” akasema Rais Ruto.
Alijinadi kuwa viwanda 17 vya sukari kote nchini sasa vinafanya kazi huku viwanda vingine vinne navyo vikiendelea kujengwa. Alitaja kuimarishwa kwa kiwango cha mpunga na kahawa ambayo imekuwa ikizalishwa kutoka mashambani.
Changamoto zinazokumba SHIF
Wakati ambapo Wakenya wamekuwa wakilalamika kuhusu changamoto zinazokumba Bima ya Afya ya Jamii, Rais alitangaza kuwa serikali italipa madeni yote kwa SHA ambayo aliirejelea kama Taifa Care ya Oktoba kufikia wiki kesho.
Madeni hayo yalirithiwa na bima hiyo mpya kutoka kwa bima ya zamani ya NHIF. Rais aliipigia debe SHA akisema kuwa itawajumuisha Wakenya wote bila kubagua iwapo wameajiriwa au la.
“Zaidi ya Wakenya milioni 50 wamejisajili Taifa Care na zaidi ya asilimia 60 ya waajiri sasa wanahakikisha wafanyakazi wao wanachangia bima hiyo,” akasema akitangaza kuwa serikali imetoa Sh3.7 bilioni kulipa madeni ambayo ilikuwa ikidaiwa na hospitali mbalimbali.
Kati ya mradi ambao utawala wa Kenya Kwanza ulikumbatia kwa kishindo ni ule wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu. Kiongozi wa nchi alitangaza kuwa nyumba 4,888 zimekamilishwa na Wakenya sasa wako huru kuzinunua.
“Mchakato wa kupata nyumba hizi utakuwa na uwazi ili kila Mkenya awe na nafasi ya kumiliki nyumba. Kila Mkenya ambaye ametimiza umri wa miaka 18 yupo huru kujadiliana na maafisa wetu nyanjani kununua nyumba hizi,”
Katika utoaji ajira, tangu Julai 2023, Wakenya 105, 367 wamepata nafasi za kazi katika mataifa mbalimbali ya nje kutokanana msaada wa serikali. Rais alifichua kuwa kwa sasa kuna nafasi 560,000 ambazo ziko wazi kwa wale ambao wangetaka waajiriwe nje ya nchi.
Nchi hizo Uingereza, Canada, Ujerumani, Mmliki ya Kiarabu, Kuwait, Saudi Arabia, Qatar, Oman, Australia na Bahrain. Serikali pia bado inazungumza na Urusi, Poland na Jordan ili kupata nafasi za ajira kwa Wakenya katika mataifa hayo.
Rais pia alilaani mauaji yanayoendelea dhidi ya wanawake, utekaji nyara uliokithiri na ufisadi. Aliwaahidi Wakenya kuwa ataendelea kupambana vikali na ufisadi na wakati huo huo kusema nyingi za huduma za serikali sasa zinapatikana mitandaoni.