Habari za Kitaifa

Ruto ageuza Homa Bay makao makuu ya Serikali Jumuishi akifanya ziara zaidi ya 10

Na RUSHDIE OUDIA, GEORGE ODIWUOR, COLLINS OMULO August 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KAUNTI ya Homa Bay ambayo kwa miaka mingi imekuwa kitovu cha siasa za uasi imegeuka himaya na makao mapya ya Rais William Ruto huku siasa za uchaguzi mkuu wa 2027 zikiendelea kunoga.

Wakati huu ambapo Rais yuko katika Serikali Jumuishi na Kinara wa ODM Raila Odinga, amekuwa akizuru kaunti hiyo mara kwa mara na kujipigia debe, idadi ya ziara zote ikiwemo hafla za matanga, rasmi na kisiasa ikiwa zaidi ya 10.

Ziara hizo tayari zimeibua madai kuwa Gavana Gladys Wanga huenda akawa mgombea mwenza wake katika uchaguzi mkuu ujao.

Tangu azuru Homa Bay kwa mara ya kwanza akiwa rais mnamo Oktoba 2022 na Februari 2025, Rais amekuwa katika kaunti hiyo mara sita kwa shughuli rasmi.

“Ninashukuru kwamba nimerejea Homa Bay, kaunti ambayo ina uwezo mkubwa katika nyanja mbalimbali.

“Tunaposherehekea matunda ya ugatuzi, Homa Bay ni mfano wa ufanisi huo,” akasema Rais alipofungua Kongamano la Ugatuzi linaloendelea Homa Bay, Jumatano.

Alionekana kuwa ‘nyumbani’ mjini Homa Bay ambako aliwasili Jumanne na hata kukutana na viongozi wa kike katika Ikulu ndogo ya Homa Bay.

Ikulu hiyo ilijengwa na serikali kuelekea katika maadhimisho ya Sherehe ya Madaraka Dei mwaka huu.

Rais Ruto alitembelea Homa Bay mara ya kwanza Oktoba 2, 2022 ambako alihudhuria ibada katika Kanisa la African Inland mjini Homa Bay.

Mnamo Januari 2023 alirejea Homa Bay kuzindua miradi ya ujenzi wa nyumba za gharama nafuu pamoja na kuzindua ujenzi wa soko la Homa Bay.

Mnamo Julai mwaka huo, kiongozi wa nchi alikuwa nyumbani kwa Katibu katika Wizara ya Usalama wa Ndani Raymond Omollo, Kanyipir eneobunge la Karachuonyo kwa maombi ya shukrani.

Baadaye Oktoba, alitembelea Kisiwa cha Mfangano ambapo pia alizuru mashamba ya Victory Sindo kabla ya kufungua afisi ya UDA mjini Homa Bay.

Mnamo Agosti 2024, Rais Ruto alikuwa Homa Bay ambako aliahidi kufanya mji huo kuwa kati ya majiji nchini.

“Tunapanga kuweka Homa Bay kuwa jiji na nitahakikisha kuwa hilo linafanyika,” akasema Rais Ruto.

“Utawala wangu unamakinika kuhakikisha sekta zote na mihimili yote ya uchumi Homa Bay inanawiri. Hii inajumuisha kawi, usambazaji wa maji, barabara, biashara na kukamilishwa kwa uwanja wa Raila Odinga,” akaongeza.

Wakati wa ziara hiyo alikagua ujenzi wa soko la samaki Homa Bay.

“Nitarudi Desemba kufungua soko hili na umeme utaunganishwa kuhakikisha wakulima wanafanya biashara zao bila tatizo lolote,” akasema Rais Ruto.

Mnamo Desemba 2024, Rais Ruto alirejea Homa Bay akiwa ameandamana na kigogo wa siasa za Nyanza, Bw Odinga kuhudhuria kipute cha soka cha Kombe la Gavana maarufu kama Genowa.

Ziara hizo za Homa Bay sasa zinazidi idadi ambayo mtangulizi wake Uhuru Kenyatta alitembelea kaunti hiyo kwa miaka 10 ambayo alikuwa mamlakani.

Rais Uhuru aliyependa zaidi Kaunti ya Kisumu, hakufikisha idadi hiyo ya ziara kwa kipindi cha miaka minne tangu aridhiane na Bw Odinga kupitia handisheki.

Februari mwaka huu, Rais Ruto alikuwa mgeni wa heshima katika Kongamano la pili la Kimataifa kuhusu Uwekezaji la Kaunti hiyo katika Chuo Kikuu cha Tom Mboya.

“Ni vigumu sana kumchukia (Gavana) Wanga. Sikuwa na pahala popote pa kujificha. Nitarudi mwaka ujao kwa sherehe za Mashujaa,” akasema Rais Ruto.

Alitimiza ahadi hiyo aliporejea miezi minne baadaye kwa ziara yake nyingine kwa sherehe ya Madaraka Dei.

Jana, Gavana Wanga alisema ziara za Rais Ruto katika kaunti hiyo zimesaidia katika kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo na mingine bado inakuja.

Katika ngome ya Bw Odinga ya Luo Nyanza, Rais Ruto anaonekana kuwa na watetezi sugu pia Homa Bay ambao wamekuwa wakisisitiza kuwa eneo hilo haliko tayari kuondoka ndani ya Serikali Jumuishi.