Ruto ahakikishia ODM atakubali masharti yao mradi wawe pamoja 2027
RAIS William Ruto amesema kuwa utawala wake utazingatia masharti yanayosukumwa na ODM kuelekea uchaguzi wa 2027, akisema chama hicho kinastahili kujiandaa kuwa ndani ya serikali inayokuja.
Kiongozi wa nchi alionyesha imani kuwa washindani wake hasa Kinara wa Wiper Kalonzo Musyoka, hawatamshinda katika uchaguzi huo.
Alisema ana ajenda kwa nchi hii na kwamba rekodi yake ya maendeleo inajizungumzia ndiyo maana wapigakura watamchagua badala ya Bw Musyoka.
“Huwezi kuongoza nchi kama huna ajenda kwa raia na yeyote asiye na rekodi ya maendeleo hafai kupigiwa kura. Watu wengine wamekuwa uongozini kwa miaka 40 lakini hawawezi kuwaambia Wakenya kile ambacho walifanya katika kipindi hicho au mipango yao,” akasema Rais Ruto.
Alikuwa akiongea katika Shule ya Msingi ya Kadika, Migori wakati wa kukamilika kwa mashindano ya soka yaliyodhaminiwa na mbunge wa eneo hilo Junet Mohamed.
Baadhi ya wanachama wa ODM wamekuwa wakimwekea Rais Ruto masharti kabla ya kuamua kuunga au kutounga azma yake ya kipindi cha pili uongozini 2027.
Kati ya masharti hayo ni nyadhifa za ziada za uwaziri na mapendeleo kisiasa. Baadhi ya viongozi wa ODM nao wamekuwa wakisema wanataka mazungumzo mengine na rais.
Bw Mohamed, Kiongozi wa ODM Dkt Oburu Oginga na Mwenyekiti wa Kitaifa Gladys Wanga, waliandamana na Rais lakini walikosa kuzungumzia matakwa hayo hadharani.
Hata hivyo, rais aliamua kujibu matakwa ambayo wamekuwa wakiyaitisha, akisema hatawacha ODM nyuma kwenye uchaguzi wa 2027.
“Kuweni tayari. Nitaandaa kikosi changu kisha tukutane na tuunde Serikali Jumuishi.”
“Msiwe na wasiwasi dhidi ya washindani wetu kwa sababu nawajua vizuri. Kama huna rekodi ya maendeleo au huwezi kueleza raia kile ulichofanya kwa kipindi kirefu umekuwa uongozini, basi sahau kuwa kiongozi wa Kenya,” akasema.
Kwa mujibu wa Rais, Kenya imesalia nyuma kimaendeleo kwa sababu viongozi waliokuwa madarakani hapo awali hawakuwa wakichangamkia maendeleo ya raia.
“Niko tayari kuzungumzia rekodi yangu na mipango ambayo ninayo kwa nchi hii. Tutatembea safari hii pamoja mwaka ujao,” akasema.
Bw Mohamed alisema ODM itaendelea kuwa serikalini na kuwa wao wanalenga siasa za 2032 kwa sababu 2027 itakuwa mswaki kwa Rais Ruto.
Alilalamika kuwa baadhi ya viongozi wa ODM ni wasaliti na hawana heshima tena kwa uongozi wa chama hicho kilichokuwa kikiongozwa awali na marehemu Raila Odinga.
“Kile ambacho kiongozi wetu Dkt Oburu Oginga atakisema ndicho tutakifuata. Watakaompinga watajipata nje,” akasema Bw Mohamed.
Alimshutumu Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta kwa kuhusika na mzozo wa uongozi unaoendelea ODM lakini akasisitiza kuwa chama kitasalia imara.
“Oburu ana watu wake na tutamtetea. Wengine wakisema kuwa ODM itakuwa na mwaniaji wa urais 2027 basi mtu huyo ni Oburu na mwelekeo wowote utatoka kwake,” akasema mbunge huyo wa Suna Mashariki akifichua kuna mpango wa kupambana na waasi wa chama mwaka ujao.
Akizungumza kwenye hafla hiyo Dkt Oginga alisema kila kitu anachofanya ODM kingefanywa na marehemu kakake Raila.
Alisisitiza kuwa licha ya umri wake pevu wa miaka 82 bado ana nguvu za kuongoza ODM.
“Sitatetereka na yeyote anayefikiria nitakufa hivi karibuni, atashangaa. Nipo,” akasema akijilinganisha na rais wa Amerika Donald Trump ambaye ana umri sawa naye.
Mawaziri Wycliffe Oparanya (vyama vya ushirika), John Mbadi (Fedha), Hassan Joho (Uchumi samawati) na Opiyo Wandayi (Kawi) walihudhuria hafla hiyo.
Bw Joho alisema atamuunga mkono Rais mnamo 2027 akisema kuwa yeye bado ni mwanachama wa ODM.