Habari za Kitaifa

Ruto ainyenyekea mahakama aruhusiwe kukata ushuru wa nyumba

January 4th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA SAM KIPLAGAT

RAIS William Ruto mnamo Jumanne aliirai Mahakama ya Rufaa kuiruhusu serikali yake kuendelea kukusanya ada tata za makato ya nyumba, ikingoja kusikilizwa kwa rufaa inayopinga utekelezaji wake.

Kupitia Mwanasheria Mkuu Justin Muturi, Dkt Ruto alisema kuwa kupitia mpango wake wa kujenga nyumba za bei nafuu, serikali imebuni ajira 120,000 na inalenga kujenga jumla ya nyumba 258,874 kila mwaka.

Alisema huenda mpango huo ukakosa kutimia ikiwa mahakama itasimamisha ukusanyaji wa ada hiyo.

Mwaka 2023, Mahakama Kuu ilitoa uamuzi kwamba utekelezaji wa ada hiyo ni kinyume cha sheria, kwani unawalenga watu wenye ajira rasmi pekee, huku wale wasio na ajira rasmi wakikosa kutozwa.

Hata hivyo, majaji watatu walisimamisha uamuzi huo hadi Januari 10, 2024, ili kuipa serikali nafasi kukata rufaa dhidi ya uamuzi huo.

Mnamo Jumatano, Bw Muturi aliwaambia Majaji wa Mahakama ya Rufaa Hannah Okwengu, John Mativo, na Mwaniki Gachoka, kuwa kwa miezi sita tangu ada hiyo ilipoanza kutekelezwa, kuna hatua nyingi zilizofikiwa, zikiwemo upatikanaji wa fedha nyingi kwa utekelezaji wa mpango huo.

Bw Muturi alisema kuwa tayari, nyumba 39,879 zishazinduliwa, huku nyingine zipatazo 32,420 zikitarajiwa kuzinduliwa baada ya ujenzi wake kukamilka.

“Miradi iliyoanzishwa kutokana na mpango wa ujenzi wa nyumba za bei rahisi kwa umma inaendelea kutekelezwa. Ikiwa mpango huo utasimamishwa, basi utekelezaji wake utavurugika, hali ambayo pia itatuathiri pakubwa kiuchumi,” akasema Bw Muturi, kwenye mawasilisho yake kwa mahakama.