• Nairobi
  • Last Updated June 15th, 2024 1:54 PM
Ruto ajibu maswali ya mbolea feki ziarani Amerika

Ruto ajibu maswali ya mbolea feki ziarani Amerika

NA MARY WANGARI

SAKATA inayohusu mbolea feki ambayo wakulima walisambaziwa kupitia Bodi ya Nafaka na Mazao Nchini (NCPB) ilionekana kupenya hadi nchini Amerika, baada ya Mkenya anayeishi nchini humo kumueleza Rais William Ruto jinsi alivyoachwa akikadiria hasara ya Sh250,000.

Bw Charles Mongosi, ambaye ni mkazi wa jiji la New York City na ambaye ni mkulima anayemiliki ekari kadhaa za ngano katika Kaunti ya Narok, alisema kuwa alipoteza maelfu hayo baada ya kununua mbolea feki.

Alisema hayo wakati Dkt Ruto alishiriki kikao maalum na Wakenya wanaoishi Amerika, wakati wa ziara yake rasmi nchini humo.

“Mimi ni mkulima anayeishi nje ya Kenya. Najua ulipata habari kuhusu mbolea feki tuliyouziwa na NCPB. Kuanzia afisi yako na Wizara ya Kilimo, mfahamu kwamba wakulima tunateseka,” alisema Bw Mongosi.

Alisema anadai fidia ya takriban magunia 100 ya mbolea.

Akijibu swali lake, Dkt Ruto alisema kuwa serikali imeanzisha mchakato wa kuwafidia wakulima wasiopungua 7,000 waliojiandikisha wakilalamikia kuuziwa mbolea feki.

“Tuliagiza kila mkulima aliyenunua mbolea iliyogunduliwa hatimaye kuwa mbovu ambapo wakulima 7,000 walijisajili. Tayari tumeanza mchakato wa kumfidia kila mkulima, utapata kiasi sawa na ulichokuwa umenunua bila kulipa,” akasema Dkt Ruto.

Aidha, Kiongozi wa Taifa alisema kuwa, “mkurugenzi wa NCPB na timu yote sasa wanasubiri kushtakiwa. Tayari tumewatimua afisini na tutawachukulia hatua kali.”

“Kando na kuwafidia mliouziwa mbolea ghushi, tutakabiliana vilevile na wahalifu.”

Haya yakijiri, Waziri wa Kilimo Mithika Linturi alidokeza Jumatano kuhusu uwezekano wa kurejelea usambazaji wa mbolea ya bei nafuu kwa wakulima, akisema serikali imetoa pesa inazodaiwa na mashirika ya kusambaza mbolea hiyo.

Waziri Linturi alisema serikali imeachilia Sh3 bilioni za kuwalipa wasambazaji wa bidhaa hiyo inayohitajika mno na wakulima hasa msimu huu wa upanzi, alipofikka jana katika Bunge la Seneti wakati wa kipindi cha maswali.

Serikali mnamo Aprili ilipiga marufuku usambazaji mbolea ya bei nafuu kupitia Kampuni ya KEL Chemicals huku ikiagiza wakulima kununua bidhaa hiyo katika mabohari yake ya NCPB.

Hatua hii ilifuatia kilio cha wakulima katika maeneo kadhaa nchini wakilalamikia kuuziwa mbolea feki.

Akijibu Seneta wa Kaunti ya Marsabit kuhusu kufidia jamii za wafugaji waliopata hasara baada ya mifugo yao kusombwa na mafuriko, Bw Linturi alisema inasubiri orodha kamili ya walioathiriwa.

“Hatuwezi kulipa fidia kijumla tu bila kutathmini kwa kina kila kisa binafsi. Tunahitaji kujua ni nani aliyeathirika na kwa kiwango kipi,” alisema Bw Linturi.

“Sh500 milioni zinadhamiriwa kulinda jamii za wafugaji dhidi ya majanga ya kimaumbile kama vile mafuriko na kiangazi. Ikiwa Bunge litapitisha pendekezo hilo katika bajeti kuu na ya ziada, jamii za wafugaji zitanufaika kuanzia mwaka 2024.”

Aidha, aliwashutumu maafisa wakuu serikalini wanaokataa kulipa baada ya kukopa maelfu ya pesa kutoka kwa Taasisi ya Kufadhili Kilimo (AFC).

“Hivi karibuni nitaachilia orodha ya kuwaanika viongozi mashuhuri serikalini, wakiwemo magavana na maseneta, ambao wamekopa na hawataki kulipa. Hatuna tatizo kukopesha lakini ukikopa sharti ulipe. Fedha hizo zinakusudiwa kufadhili shughuli za kilimo. Tukianza kufuatilia malipo, watu wanaanza kulia eti wanaandamwa.”

  • Tags

You can share this post!

Stivo Simple Boy: Nilivalia jeans ya Kiafrika ya Sh237,600...

Wakulima waliopoteza mazao kwa mafuriko kukosa fidia

T L