Habari za Kitaifa

Ruto ajipanga upya kuteka Mlima: Ushindi Mbeere Kaskazini wampa shavu

Na MOSES NYAMORI January 14th, 2026 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto sasa anaonekana kuzidisha juhudi za kuwinda kura za Mlima Kenya akikumbatia mbinu mbalimbali kurejesha eneo hilo kwenye himaya yake kisiasa kuelekea 2027.

Hii ni baada ya miezi kadhaa ya kukwepa eneo hilo kutokana na uhasama wa kisiasa kati yake na aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.

Mlima ambao ulimpigia kura kwa fujo Rais Ruto mnamo 2022 ulionekana kuanza kumponyoka baada ya kuondolewa kwa Bw Gachagua madarakani mnamo Oktoba 2024.

Baada ya kutimuliwa kwa Bw Gachagua, Rais Ruto alikwepa mlima huku wandani wake wakikabiliwa vikali na kupokea upinzani kutoka wakazi wa eneo hilo.

Hata hivyo, ushindi katika uchaguzi mdogo wa Mbeere Kaskazini Kaunti ya Embu umempa Rais motisha kwamba, bado ana nafasi mlimani, eneo lililompa karibu kura milioni tatu 2022.

Uchaguzi wa mashinani wa UDA, mikutano yake ya kisiasa inayoendelea kushika kasi na kuzinduliwa kwa miradi mingi ya serikali ni kati ya mikakati ambayo Kenya Kwanza sasa inatumia kupenya mlimani.

UDA Jumamosi iliandaa uchaguzi wake wa mashinani Mlima Kenya bila upinzani wowote. Maafisa 20 waliochaguliwa kwenye kila kituo cha upigaji kura wanatarajiwa kuvumisha chama mashinani na kumtafutia Rais kura.

Kaunti 10 za Mlima Kenya na saba za Kaskazini mwa Bonde la Ufa zilichangia zaidi ya kura milioni 4.5 za Rais Ruto hii ikiwa ni asilimia 63 za kura zote alizopata.

Kaunti za Laikipia, Tharaka-Nithi, Murang’a, Kiambu, Nyeri, Kirinyaga, Nyandarua, Embu, Meru na Nakuru ambazo ni za Mlima Kenya zilimpa Rais karibu kura milioni tatu.

Ushindi Mbeere Kaskazini umesaidia kubadilisha dhana kuwa Rais Ruto alikuwa ameisha nguvu kisiasa na Bw Gachagua kutwaa ubabe.

Hii ni kwa sababu Rais amekuwa akiandamwa na changamoto si haba hasa baada ya maandamano yaliyoendelezwa na Gen z mnamo 2024 na 2025.

Mnamo Jumatatu, Rais Ruto alikuwa Kaunti ya Nyeri ambapo alikanusha vikali madai ya Bw Gachagua kuwa alimsaidia kupata kura za mlima.

Aliyekuwa naibu rais amekuwa akiwaambia wenyeji wa eneo hilo kuwa ndiye alimtambulisha rais kwao kuelekea 2022.

“Sikujua Ruto atakuwa hivi na naomba msamaha kwa kuwaelekeza vibaya. Sasa tunamjua na hatutampa kura zetu,” akasema Bw Gachagua.

Hata hivyo, Rais anasema hakuna anayefaa kujifanya alichangia umaarufu wake Mlima Kenya akisisitiza alipendwa kwa kuzindua miradi ya maendeleo akiandamana na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta.

“Nimesikia baadhi ya watu wakisema walinibeba mgongoni na kunitambulisha kwa Mlima. Hakuna aliyenileta hapa na ukweli ni kwamba nilikuwa naandamana na bosi wangu Uhuru Kenyatta ama alikuwa akinituma kuzindua miradi ya maendeleo eneo hili,” akasema Rais akiwa Kaunti ya Nyeri ngome ya kisiasa ya Bw Gachagua.

“Wakati nilikuwa naibu rais, nilizindua miradi na kuwakilisha bosi wangu. Nilizindua ujenzi wa makanisa, barabara kutokana na urafiki wetu wa zaidi ya miaka 20. Yeyote anayedai alinitambulisha kwenu asifikirie atavunja urafiki wetu,” akaongeza akiwa eneobunge la Othaya Jumapili.

Rais alitoa matamshi hayo tena mjini Nyeri alipozindua ujenzi wa madarasa katika Shule ya Msingi ya Nyamachaki na pia akakagua ujenzi wa bararabara ya Kenol-Marua.

“Wajue kuwa hawatanitisha kwa kusema muhula mmoja hata wakiniita Kasongo. Hawana ajenda ya kuwaambia Wakenya kuhusu 2027 na atakayechaguliwa ni yule ameonyesha rekodi ya kuwapa raia maendeleo,” akasema.

Hata hivyo, Mbunge wa Gatanga Edward Muriu, mwandani wa Bw Gachagua, anasema kuwa mapokezi ambayo Rais Ruto aliyapata yalikuwa baridi na hayawezi kulinganishwa na 2022.

“Amerudi mlimani akiwa na majuto mengi kwa sababu anajua mambo yaliharibika baada ya kuwasaliti. Kama kiongozi,lazima apambane na kuonyesha ujasiri kuwa kila kitu kiko shwari hata kwa njia ya kujifanya,” akasema Bw Muriu.

Mbunge huyo alidai kuwa baadhi ya waliofika kwa mikutano ya Rais ni wale waliokodishwa na kulipwa.

“Watu wa Mlima huwa si wa fujo, hawazomei viongozi au kurusha mawe. Watamsikiza Ruto na miradi yake lakini debeni, kura zao hatazipata,” akaongeza.

Alisema miradi inayozinduliwa au kuendelezwa na rais haiwezi kuwahadaa warejee kambini mwake kwa sababu baadhi hata ilizinduliwa Bw Kenyatta akiwa mamlakani.

“Huenda kwa sasa wasijue watakayempa kura zao 2027 lakini wanajua hawatampa Ruto. Watu walihama kutoka kwake mapema sana na wanasubiri tu kura kumtuma nyumbani,” akasema.

Seneta wa Kitui Enoch Wambua naye anasema wakazi wa Mlima Kenya wana sababu zenye mashiko za kumtoroka Rais Ruto.

“Amewafuta mabinti na watoto wao kutoka Baraza la Mawaziri bila sababu na pia ameharibu uchumi na kusambaratisha biashara zao. Alihakikisha naibu wake anafurushwa kinyume na matakwa ya jamii na utawala wake umewanyanyasa na kuwadhulumu vijana,” akasema Bw Wambua.

Seneta huyo anasema Mlima Kenya umekuwa na marais watatu kati ya watano na hawana chochote cha kujivunia au kufurahia kuhusu urais wa Ruto.

“Amewadhulumu na ingawa siwezi kuzungumza kwa niaba yao, sidhani kama watampigia kura 2027,” akasema.