• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 8:50 AM
Ruto akaidi Amerika kuhusu marufuku dhidi ya shughuli za WorldCoin

Ruto akaidi Amerika kuhusu marufuku dhidi ya shughuli za WorldCoin

NA EDWIN MUTAI

KENYA imekataa shinikizo kutoka kwa serikali ya Amerika kuhusu kuondoa marufuku dhidi ya mradi wa uwekezaji kidijitali alamaarufu WorldCoin, wabunge wameelezwa.

Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki alieleza Bunge jana kuwa serikali haitaondoa marufuku yaliyotangazwa Agosti 2023, dhidi ya shughuli za WorldCoin.

Alipofika mbele ya Kamati ya Bunge la Kitaifa kuhusu Malalamishi ya Umma, Profesa Kindiki alisema Kenya imekuwa ikishinikizwa na serikali ya Amerika kufutilia mbali marufuku hayo.
“Amerika imekuwa ikishinikiza serikali kuhusu masuala ya WorldCoin lakini tumesalia imara na wakakamavu,” alisema Profesa Kindiki.

“Wanafikiri (Amerika) kuwa bado wana (WorldCoin) nafasi ya kuendesha shughuli zao hapa. Tumesalia imara na msimamo wetu utabaki hivyo. Hatutabatilisha marufuku hayo.”

Prof Kindiki alifika mbele ya Kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Kuria Mashariki, Marwa Gitayama, na ambayo inaandaa nakala ya malalamishi ya umma yanayolenga kupiga marufuku mtandao maarufu wa China, Tiktok.

Alisema serikali inatathmini mbinu zozote ikiwemo kupunguza baadhi ya shughuli za TikTok jinsi ilivyokuwa na WorldCoin ambapo serikali imeendelea kukataa shinikizo za Amerika kuhusu kuondoa marufuku dhidi ya kukusanya data ya mboni za raia Wakenya.

Mnamo Agosti 2, 2023, Profesa Kindiki alitoa amri iliyositisha shughuli zote za WorldCoin akisubiri uchunguzi kukamilishwa kuhusu kubaini usalama wa data inayokusanywa.

Wakati huo, Prof Kindiki alisema marufuku hayo yataendela hadi hakikisho la usalama na uadilifu kuhusu mikataba ya kifedha itakapotolewa.

“Serikali imezima shughuli za WorldCoin na shirika lingine lolote linahusisha watu wa Kenya hadi mashirika husika ya umma yatakapothibitisha hakuna hatari yoyote kwa umma,” alisema Waziri kupitia taarifa.

  • Tags

You can share this post!

Si lazima ujengewe nyumba ‘ushago’, mke wa pasta...

Juhudi za Kalonzo kujivua ‘mikosi’ ya Raila

T L