Habari za Kitaifa

Ruto akemea wabunge wa Kenya Kwanza wanaopinga sera zake

February 19th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

Na KENNEDY KIMANTHI

RAIS William Ruto Jumatatu alikemea vikali wabunge wa Kenya Kwanza wanaokosoa sera zake za uongozi akionya kwamba huenda wanajihatarisha kisiasa kabla ya Uchaguzi Mkuu 2027.

Rais aliwazomea wabunge hao kwa kukosa kupigia debe sera za Kenya Kwanza hasa kuhusu Mpango wa Nyumba za Bei Nafuu na Mpango wa Afya kwa Wote akiwaagiza kuanza kufanya hivyo mara moja.

Kiongozi wa Taifa alisema haya katika warsha ya Uongozi wa Kitaifa na Kundi la Bunge inayoendelea Naivasha, jijini Nakuru.

Kauli yake ilichochewa na madai kuwa baadhi ya wabunge waliomo serikalini wanamhujumu Rais ilhali kwa kawaida, waundasheria husimama pamoja kulinda misimamo na sera za vyama bungeni.

Dkt Ruto ambaye umaarufu wake unaonekana kufifia mashinani kutokana na hali ya kiuchumi, alisema angali imara kama kiongozi wa wabunge wa Kenya Kwanza na yupo makini kuzima migawanyiko yoyote katika kambi yake.

“Nataka kuwaagiza wabunge kutilia maanani baadhi ya mambo wanayofanya kwa sababu tunaandaa mitihani ya 2027. Mmedokezewa mtihani na mtakachofanya na hilo ni shauri yenu. Ni sharti niwakumbushe mimi ni mtu mwenye malengo na ninamaanisha na watu wanafaa kufuatilia kwa makini. Hakuna serikali ingine Bungeni, ni wabunge wetu na nyinyi ndio serikali, kwa hivyo acheni kuashiria kidole serikali nyingine. Hata msiwaze kwamba kuna serikali nyingine,” Dkt Ruto aliwaeleza wabunge wa Kenya Kwanza.