Habari za Kitaifa

Ruto alaani ukabila na ubaguzi katika hotuba iliyoonekana kuelekezewa Gachagua

Na SIAGO CECE, VALENTINE OBARA October 21st, 2024 Kusoma ni dakika: 2

RAIS William Ruto amelaani migawanyiko ya kikabila inayoshuhudiwa nchini na kuwataka wanasiasa kukomesha siasa zinazolenga kubagua maeneo mengine kimaendeleo.

Akiongea Jumapili katika Uwanja wa Michezo wa Kwale wakati wa Sherehe za Mashajaa Dei, Dkt Ruto alisema mashujaa wa uhuru hawakupigania maslahi ya makabila yao bali ya Wakenya wote.

Alisema viongozi wa sasa wanafaa kukumbatia moyo wa mashujaa hao kwa kutetea na kuendelea maslahi ya raia wote wala sio makabila au maeneo wanakotoka pekee.

“Alipopigana na ukoloni, Mekatilili wa Menza hakulenga kuleta uhuru katika kijiji, eneo au jamii yake pekee. Badala yake alipinga unyanyasaji na udikteta wa mkoloni kwa imani kwamba akishinda taifa lote lingekuwa huru. Huu ndio moyo uliokumbatiwa na mashujaa wengine wa uhuru,” akasema.

Ingawa Rais Ruto hakumtaja moja kwa moja naibu rais Rigathi Gachagua kauli yake na maneno yake yalionekana kupinga madai ya Gachagua kwamba yeye ni mpiganiaji wa maslahi ya ngome yake ya kisiasa ya Mlima Kenya.

Kabla ya kuondolewa mamlakani wiki jana, Bw Gachagua amekuwa akiendesha kampeni ya kutaka eneo hilo litengewe mgao mkubwa wa mapato ya kitaifa kwa misingi ya kura nyingi za wakazi zilizouwezesha muungano wa Kenya Kwanza kuingia mamlakani.

Eneo hilo na Bonde la Ufa zilichangia idadi kubwa ya kura milioni 7.1 zilizomwezesha Rais Ruto kushinda urais.

Vile vile, Bw Gachagua amekuwa akipendeleza kuwa mgao wa fedha kwa kaunti na maeneo bunge ufanywe kwa kuzingatia wingi wa watu; mfumo unaojulikana; ‘mtu-mmoja, kura-moja, shilingi-moja.’

Hudai kuwa mfumo wa sasa haulitendei haki eneo la Kati mwa Kenya lenye idadi kubwa ya watu.

Hatua yake ya kupigania masilahi ya eneo la Mlima Kenya ilitajwa kama mmoja ya mashtaka 11 yaliyoorodheshwa katika hoja ya kumtimua afisini iliyodhaminiwa na Mbunge wa Kibwezi Magharibi Mwengi Mutuse.

Bw Gachagua alikosolewa kwa kutoonyesha sifa za kiongozi wa kitaifa licha ya kushikilia wadhifa mkubwa wa naibu rais.

Jana, Rais Ruto aliwataka Wakenya kuiga mfano wa wapiganiaji uhuru kwa kuzingatia usawa.

“Funzo hili kuu limepitishwa kwetu kutoka enzi za wazee na ambalo linapasa kupitishwa kwa vizazi vijavyo. Kwa kila raia ni sawa machoni mwa viongozi wa kisiasa na anayo haki ya kufaidi kutokana na mipango yote ya maendeleo.

“Mtu fulani hafai kubaguliwa huku mwingine akipendelewa. Kwa hivyo, mfumo wowote unaolenga kutenga na kupokonya haki ya mtu, kundi au jamii yoyote, kwa sababu yoyote ile, hautakubaliwa kwani unahujumu utaifa wetu,” akasema.

Kuondolewa mamlakani kwa Bw Gachagua kuliacha pengo ambalo lilidhihirika katika sherehe ya kitaifa ya Mashujaa Dei.

Kama kawaida, naibu rais ndiye humkaribisha Rais anapowasili katika sherehe za kitaifa. Aidha, humwalika kulihutubia taifa.

Lakini katika sherehe za jana, Waziri wa Usalama Kithure Kindiki, ambaye uteuzi wake kuwa Naibu Rais ulipitishwa na Bunge la Kitaifa Ijumaa, ndiye alimkaribisha Rais Ruto katika uwanja wa michezo wa Kwale.

Kinyume na magari ya mawaziri wengine gari ambalo Profesa Kindiki alitumia liliruhusiwa kuingia ndani ya uwanja.

Aidha, alitambulishwa kama Naibu Rais Mteule.

Profesa Kindiki aliwasili pamoja na Mkuu wa Mawaziri Musalia Mudavadi aliyetwikwa kibarua cha kumwalika Rais Ruto alihutubie taifa.

Kwenye hutoba yake fupi, Bw Mudavadi pia alimtambua Profesa Kindiki kama Naibu Rais Mteule na kuwahakikishia wananchi kuwa hali ni shwari serikalini na hamna pengo lolote la uongozi.