Habari za Kitaifa

Ruto aongoza kwa umaarufu wa wawaniaji urais kura za 2027 – Utafiti

Na FATUMA BARIKI December 28th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto atashinda muhula wa pili iwapo uchaguzi wa urais ungefanyika hivi leo, hii ni kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na kampuni ya Infotrak.

Kulingana na utafiti huo kwa jina ‘End-Year Poll Politics’, Rais Ruto anaongoza kwa umaarufu kwa asilimia 28 akifuatwa na aliyekuwa Waziri wa Usalama Fred Matiang’i (asilimia 13) naye Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka ataibuka wa tatu kwa asilimia 12.

Mwanasiasa barobaro Babu Owino anashikilia nafasi ya tatu kwa asilimia 7 huku mkosoaji mkuu wa Ruto, naibu wake wa zamani Rigathi Gachagua aliyeibuka na kauli mbiu ya ‘Ruto Wantam’ anafuata kwa asilimia 5.

Hata hivyo, kutawazwa mshindi kwa kura ya urais nchini ni sharti mwaniaji apate asilimia 50+1 ya kura halali zilizopigwa na kwa sababu hiyo, inamaanisha kwamba kungehitajika awamu ya pili ya kura iwapo matokeo yatakuwa kama yalivyotabiriwa na utafiti huu.

Rais William Ruto ameonekana kupanda kwenye umaarufu haswa baada ya kuridhia kufanya kazi na aliyekuwa Waziri Mkuu na Kiongozi wa ODM marehemu Raila Odinga, hali iliyosaidia kudhibiti serikali yake iliyokuwa inakumbwa na msukosuko uliochangiwa na maandamano ya Gen Z mwaka  wa 2024.

Umaarufu wake vile vile unaonekana kuchupa zaidi katika siku za hivi punde kufuatia ushindi mnene kwenye uchaguzi mdogo Novemba ambapo wawaniaji wa Serikali Jumuishi kwenye ngazi za useneta na ubunge wote walishinda viti walivyowania; jambo lililoipa pigo kali mrengo wa upinzani unaojumuisha aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua, Kalonzo Musyoka na Fred Matiang’i uliokuwa unaimba wimbo wa ‘wantam’.