Ruto apanga kubomoa Matiang’i Gusiiland kwa kumwaga hela za maendeleo
MIRADI ya maendeleo ambayo Serikali Kuu inatekeleza katika eneo la Gusii inachukuliwa kama ya chambo cha kuwavutia wakazi wamuunge mkono Rais William Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Wachanganuzi wanasema miradi inatumiwa kuimarisha nafasi ya Rais kupata kura katika eneo hilo wanakotoka viongozi wawili wa kisiasa ambao wametangaza azma ya kuwania urais.
Wao ni aliyekuwa Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i na Jaji Mkuu mstaafu David Maraga.
Mbali na maendeleo kama vile ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, ujenzi wa masoko na uunganishaji wa umeme, Rais Ruto pia amekuwa akiwaalika viongozi kutoka Gusii katika Ikulu ya Nairobi kama sehemu ya mikakati yake ya kuwavutia upande wake.
Mkutano wa hivi punde katika makazi hayo rasmi ya Rais ulifanyika Alhamisi wiki jana ambako Dkt Ruto aliahidi kuwa serikali itaunga mkono eneo hilo kimaendeleo huku akitoa ahadi nyingine ya kuyainua maisha ya wakazi.
Eneo hilo lilikuwa na jumla ya kura 960,000 katika uchaguzi mkuu wa 2022, kulingana na takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC).
Katikati ya mwezi jana, Kiranja wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Silvanus Osoro na wabunge Japhet Nyakundi (Kitutu Chache Kaskazini), Zaheer Jhanda (Nyaribari Chache) na Alfa Miruka (Bomachoge Chache) waliwaongoza wakazi kutoka kaunti za Kisii na Nyamira kwa ziara ya Ikulu ya Nairobi.
Walidai kuwa kutokana na ziara hiyo, serikali itatekeleza miradi mipya ya maendeleo na kufufua miradi iliyokwama.
Kabla ya mkutano huo, Rais Ruto pia alikuwa mwenyeji wa wabunge na madiwani katika Ikulu-ndogo ya Kakamega mwaka jana kabla ya kukutana nao tena katika Ikulu-ndogo ya Kisii, usiku wa kuukaribisha mwaka huu wa 2025.
Rais Ruto anaendeleza kampeni ya kulivutia upande wake eneo la Gusii na Magharibi mwa Kenya ili kufidia ushawishi alioupoteza katika ukanda wa Mlima Kenya huku kambi yake ikiwa na kiwewe kuhusu azma ya Dkt Matiang’i.
Kiongozi wa taifa pia anasaka usaidizi kutoka kwa kiongozi wa ODM Raila Odinga, ambaye kwa miaka mingi amepata uungwaji mkubwa katika eneo la Gusii.
Ndiyo maana katika mkutano wa Alhamisi kati ya Rais Ruto na viongozi wa Gusii, Bw Odinga, ambaye sasa ni mshirika wake katika Serikali Jumuishi alishiriki.
Ujumbe huo wa viongozi wa jamii hiyo uliongozwa na Gavana wa Kisii, Simba Arati na kushirikisha Waziri wa Elimu Migos Ogamba, Wakili Mkuu wa Serikali Shadrack Mose, miongoni mwa wengine.
Lakini huku Bw Arati akiongoza ujumbe huo, mwenzake wa Nyamira Amos Nyaribo hakuwepo baada ya kusemekana kuwa alikataa mwaliko huo.
Bw Nyaribo ni kiongozi wa chama cha United Progressive Alliance (UPA) kinachohusishwa na Dkt Matiang’i, ambaye ni mzaliwa wa Kaunti ya Nyamira.
Baada ya mkutano wa Ikulu Alhamisi wiki jana, Naibu Rais Prof Kithure Kindiki alifanya mkutano tofauti na madiwani wa Nyamira ambapo waliohudhuria walisema ajenda kuu ilikuwa kuimarisha chama cha United Democratic Alliance (UDA) na kuyeyusha ushawishi wa Dkt Matiang’i.
Wale waliohudhuria mkutano huo uliofanyika Ijumaa usiku waliambia Taifa Leo kuwa walijadili kuhusu chaguzi ndogo zijazo katika wadi kadhaa za Kaunti ya Nyamira.
Diwani mmoja ambaye hakutaka kujitambulisha alisema walienda kwa Prof Kindiki kuomba usaidizi kuhusu “suala” la gavana wa kaunti hiyo. Alidokeza kuhusu mipango ya kumtimua Gavana Nyaribo.
Mnamo Jumanne wiki jana, wabunge wanaoegemea mrengo wa Kenya Kwanza waliendeleza kampeni katika eneobunge la Mugirango Kaskazini na kaunti nzima ya Kisii.
Wakati wa mkutano wa wabunge hao, Mbunge wa Kitutu Chache Kaskazini Japhet Nyakundi aliwarai madiwani wa Nyamira wakimtimue Gavana Nyaribo kuwa kukataa mwaliko wa Rais Ruto.
“Mko na mamlaka na kumwondoa mtu huyo afisini ili naibu wake ashike usukani. Gavana Arati alikubali kuwapeleka madiwani Ikuluni lakini gavana wenu alikataa. Mumtimue!” Bw Nyakundi akasema.