Ruto apanga kukwamilia Raila kupata ‘nguvu’ za kukabiliana na Upinzani
RAIS William Ruto ameanza kujipanga kwa kura ya 2027 huku akianzisha mikakati ya kisiasa, kiuchumi na masuala ya kijamii kupata tikiti ya kuhudumu muhula wa pili.
Kwenye vikao mbalimbali vya umma, Rais amekuwa akisisitizia mikakati ya kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo huku ushirikiano wake na Kinara wa ODM Raila Odinga ukimvunia ujasiri wa kuukabili upinzani.
Sasa, imebainika Rais Ruto na wandani wake wameweka mipango ya kuhakikisha wanadhibiti maeneo muhimu kisiasa kisha kulemea upinzani katika ngome zake.
Duru zinaarifu Rais Ruto anamakinikia kumkwamilia Raila na wawili hao ndio wapo nyuma ya mikutano ya kuinua makundi ya kijamii kisiasa ambayo imekuwa ikiendelea nchini.
Mikutano hiyo huwa inaongozwa na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki na wanasiasa kutoka mirengo yote miwili na imekuwa ikiendelea kaunti mbalimbali nchini.
Pia, Rais analenga kuendeleza mtindo wa 2022 ambapo alishawishi makundi ya kidini na makanisa kumuunga mkono.
Pamoja na hayo, analenga kupigia debe ufanisi wa mradi wa nyumba za gharama nafuu na mageuzi kwenye idara ya afya, kilimo, kubuni nafasi za ajira kwa vijana pamoja na kuimarika kwa mfumo wa kidijitali.
Japo Raila hajaweka wazi iwapo atamuunga Rais Ruto kwa muhula wa pili, wandani wake wamekuwa wakisema hivyo huku wakisisitiza hawako tayari kushirikiana na mrengo wa aliyekuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua.
Akiwa Kuria, Kaunti ya Migori wikendi, Profesa Kindiki aliashiria kuwa hakuna wasiwasi wowote na ni jambo ambalo limethibitishwa kuwa Raila na Rais watashirikiana 2027.
Bw Odinga Jumanne aliongoza mkutano wa kamati ya ODM Nairobi ambapo suala la ushirikiano na UDA lilidaiwa lilijadiliwa.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alisema walijadili sana masuala ya usimamizi wa chama.