Habari za Kitaifa

Ruto apatia dada ya Raila kazi ya serikali, akumbuka Kidero pia

Na BENSON MATHEKA November 16th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

RAIS  William Ruto amemteua aliyekuwa Gavana wa Nairobi Evans Kidero na dadake kiongozi wa chama cha ODM  Raila Odinga, Wenwa Akinyi kuhudumu katika nyadhifa serikalini.

Dkt Kidero ameteuliwa kuwa mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi ya Shirika la Kitaifa kuhusu Biashara Kenya (KNTC) kwa muda wa miaka mitatu.

Katika kumteua Dkt Kidero, Rais alibatilisha uteuzi wa Hussein Debasso. Dkt Kidero amekuwa kwenye  baridi baada ya kushindwa katika kinyang’anyiro cha ugavana wa Homa Bay katika Uchaguzi Mkuu wa 2022.

Mwaka jana, Dkt Kidero alikuwa miongoni mwa watu ambao Rais Ruto aliteua kuwa Mawaziri Wasaidizi kabla ya uteuzi huo kufutiliwa mbali na mahakama.

“Namshukuru Mheshimiwa  Rais Ruto na ninaahidi kutoa huduma kwa kujitolea kwa watu na taifa la Kenya Ili kuongeza thamani na kuleta mabadiliko,” Dkt Kidero alisema kufuatia kuteuliwa kwake.

Katika uteuzi wa hivi punde  kupitia  notisi ya gazeti la serikali ya Novemba 15, 2024, Rais pia alimteua Dkt Wenwa kuwa Mwenyekiti wa Taasisi ya Utafiti wa Bahari na Uvuvi ya Kenya, kwa muda wa miaka mitatu.

Rais Ruto pia alimteua Dkt Thuo Mathenge kuwa mwenyekiti wa Bodi ya Shirika la Utafiti wa Kilimo na Ufugaji kwa miaka mitatu kuchukua nafasi ya Peter Weru Kinyua ambaye uteuzi wake ulibatilishwa.