Ruto apongeza mwenyekiti mpya wa AUC aliyebwaga Raila
RAIS William Ruto amekubali kushindwa kwa Kenya katika uchaguzi wa Mwenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC), akisema kwamba japo matokeo ya uchaguzi huo hayakumpendelea mgombeaji wa Kenya, “ningependa kushukuru kwa dhati uongozi mzima wa bara letu kuu.”
Rais Ruto pia alimpongeza mwenyekiti mpya wa AUC, Mahmoud Youssouf na naibu wake Selma Haddadi.
“Nina imani na tume ya AU, na Kenya inaahidi kuwa itawaunga mkono kikamilifu mnapoipeleka Tume ya Muungano wa Afrika kwenye ngazi nyingine,” Dkt Ruto aliandika kwenye akaunti yake rasmi ya X.
“Uchaguzi huu haukuwa wa watu binafsi au mataifa, ulihusu mustakabali wa Afrika. Mustakabali huo unasalia na, kwa pamoja, tutaendelea kufanya kazi kwa ajili ya Afrika iliyoungana, yenye ustawi na ushawishi katika jukwaa la kimataifa,” alisema.
Mgombeaji wa Kenya wa kiti cha uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC) Raila Odinga, alishindwa katika azma yake ya kuongoza muungano huo wa bara na Waziri wa Masuala ya kigeni wa Djibouti Mahmoud Ali Youssouf.
Bw Youssouf alimshinda Bw Odinga baada ya kupata kura 33 zinazohitajika. Raila aliondolewa baada ya duru ya sita kwa kukosa kupata kura zaidi. Katika awamu ya sita, Bw Odinga alikuwa na kura 22, huku Bw Youssouf akiwa na kura 26.
Akizungumza baada ya uchaguzi, Bw Odinga alikubali matokeo ya uchaguzi wa AUC, ambapo alikuwa akishindana na Mahmoud na aliyekuwa Waziri wa Masuala ya kigeni wa Madagascar Richard James Randriamandrato.
“Nataka kumtakia kila la heri mshindani wangu Mahamoud Ali Youssouf. Namtakia mafanikio katika kazi yake. Ninawashukuru walionipigia kura na wale ambao hawakunipigia kura kwa sababu walitumia haki zao za kidemokrasia,” Bw Odinga alisema, akisindikizwa na maafisa kadhaa wa Kenya waliokuwa wameandamana naye hadi Addis Ababa.
Alisema kukubali kwake kunapaswa kueleweka kama kujitolea kwake kwa demokrasia, akisema, “mimi mwenyewe nilikubali kushindwa. Nataka tutumie hili kama mfano wa kuimarisha demokrasia katika bara letu.”
Bw Odinga alitafakari kuhusu kampeni ya miezi kadhaa ambayo ilimfanya kusafiri kote barani Afrika kuomba kura.
“Nilijitolea kama mgombeaji, na katika miezi michache iliyopita, nimezunguka bara nikizungumza na viongozi, nikitafuta kura zao. Leo wamezungumza. Na kama ilivyo sasa, hatukufanikiwa,” alisema na kuongeza kuwa hatajali kutoa huduma zake kwa bara wakati wowote akiitwa.