Ruto arudi kuzima uasi unaotokota eneo la Mlima Kenya
RAIS William Ruto leo Alhamisi anaelekea eneo la Mlima Kenya, wakati malalamishi ya Naibu Rais Rigathi Gachagua na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta yanatishia kuchochea uasi dhidi ya serikali yake ya Kenya Kwanza.
Ziara hiyo pia inajiri wakati Bw Gachagua na viongozi wa upinzani katika Muungano wa Azimio la Umoja One Kenya kutoka kanda hiyo wanaongoza kampeni ya ugavi wa mapato kwa kutegemea idadi ya watu kupitia mfumo wa mtu mmoja- kura moja- shilingi moja, wito ambao rais anahisi unagawanya nchi.
Kaunti zinazokuza miraa na muguka – mimea ambayo ina thamani ya kiuchumi kwa kaunti za Mt Kenya Mashariki za Meru, Embu na Tharaka Nithi nazo zinalalamika baada ya viongozi wa Pwani kutishia kupiga marufuku uuzaji wa zao hilo.
Lakini huku kukiwa na hali ya wasiwasi katika eneo hilo kufuatia madai ya Naibu Rais kwamba serikali imemnyima ndege ya kijeshi na kumfanya asafiri kwa ndege ya shirika la ndege la Kenya Airways mnamo Jumanne, Rais Ruto Jumanne aliongoza kikao cha Baraza la Mawaziri ambacho kiliidhinisha kufutwa kwa deni la wakulima wa kahawa na mageuzi mengine ya sekta ya kahawa, katika jitihada za kutuliza eneo hilo kabla ya ziara ya leo.
Mkutano huo ambao pia ulihudhuriwa na Bw Gachagua uliidhinisha kufutwa kwa madeni ya kihistoria ya jumla ya Sh 6.8 bilioni zinazodaiwa wakulima wa kahawa kote nchini, hatua ambayo itafaidi pakubwa wakulima wa kahawa Mlima Kenya.
Kwa kuhofia uwezekano wa uasi, Rais Ruto pia aliingilia kati kuzima mvutano baada ya Bw Kenyatta kushutumu utawala wake kwa kumnyanyasa.
Mnamo Jumanne, Dkt Ruto Jumanne alibuni kamati, ikiongozwa na Mkuu wa Utumishi wa Umma Felix Koskei, kushughulikia mara moja masuala yote yaliyoibuliwa na rais huyo mstaafu, ikiwa ni pamoja na eneo la ofisi yake na idadi ya wafanyikazi.
Kulingana na Katibu Mkuu wa Jubilee Bw Jeremiah Kioni, “urais wa Ruto ni janga miongoni mwa watu wetu kwani amepiga marufuku mjadala wa mtu mmoja kura moja ya shilingi moja kama mfumo wa ugavi wa mapato”.
Kiongozi wa Narc Kenya, Martha Karua aliambia Taifa Leo kwamba, “utawala wa Ruto uliwadanganya wakulima wetu kwamba utawafaidi kwa kutekeleza mabadiliko kupitia ajenda ya kuanzia mashinani.
Kuanzisha ushuru wa juu ni suala jingine ambalo Rais Ruto analaumiwa kwa kuumiza Mlima Kenya, hasa wakati mchakato wa kuandaa Mswada wa Fedha wa 2024 unaendelea.
“Utawala wa Ruto unajitokeza kama ule ambao nia yake ni kuua biashara zote. Tunajaribu kumshauri kwamba asitutoze ushuru zaidi lakini yuko katika harakati za kuumiza sekta zote kwa ushuru. Aina ya ushuru anaopendekeza bila shaka utazidisha umaskini,” alisema aliyekuwa mgombea Urais Bw Peter Kenneth.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Kikuyu Bw Wachira Kiago anahisi kwamba, baadhi ya wafuasi wa Ruto wamejenga ujasiri wa kuamuru Mlima kukoma kufanya mikutano ili kupanga mwelekeo wa kisiasa.