• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 12:56 PM
Ruto ashangaa ufisadi unavyosakatwa katika asasi za serikali

Ruto ashangaa ufisadi unavyosakatwa katika asasi za serikali

NA WYCLIFFE NYABERI

RAIS William Ruto amelalamikia ufujaji wa rasilimali katika baadhi ya mashirika ya serikali, akisema jambo hilo limekuwa likipunguza kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi.

Dkt Ruto amesema kuanzia bajeti ya mwaka huu, watakuwa makini jinsi ya kutenga fedha za mashirika mbalimbali ya serikali kama njia moja ya kuhakikisha matumizi yake yanakuwa ya busara.

Akizungumza Jumatatu, Machi 18, 2024 eneo la Lolgorian, Kaunti ya Narok, alipohudhuria mazishi ya Mama Annah Tunai, ambaye alikuwa mama ya Gavana wa kwanza wa Narok Samuel Tunai, Rais aliwataka wabunge kumuunga mkono katika hatua zinazolenga kuziba mianya yoyote ya utumizi mbaya wa pesa za umma.

“Nataka niwaombe wabunge tushirikiane ili pale ambapo hatuhitaji fedha tusiweke. Taasisi zinazoweza kujisimamia, tusizipe rasilimali za ziada. Tuhakikishe kuwa kila shilingi inatumiwa ipasavyo,” Rais Ruto alisema.

Alipongeza baadhi ya serikali za kaunti zinazotumia raslimali zao kwa uadilifu na kuahidi kuendelea kufanya kazi nazo kwa ukaribu.

Rais aliwataka Wakenya kukumbatia Hazina mpya ya Bima ya Afya ya Kijamii (SHIF) akisema itasaidia pakubwa kuhakikisha kwamba hakuna anayenyimwa huduma bora za afya.

“Tunataka hata yule ambaye hana njia za kulipia bima ya afya afaidike. Katika sheria mpya tulizotunga mtu huyo atapata huduma bora za afya kupitia ushuru ambao walioajiriwa wanalipa,” alisema.

Rais alichukua fursa hiyo kuwahakikishia wakazi wa Transmara kwamba utawala wake utaboresha hali ya barabara ndani ya eneo hilo ili kurahisisha uchukuzi.

Alipigia debe mradi wa ujenzi wa nyumba za bei nafuu akisema utawapa mamia ya vijana wasio na ajira fursa ya kujikimu kimaisha.

“Tutaanza mradi wa nyumba za bei nafuu hapa hivi karibuni. Tutajenga nyumba 5,000 ambazo zitawezesha vijana 10,000 kujikimu kimaisha,” Dkt Ruto alisema.

Pia aliahidi kuwa serikali yake itafanya bidii zaidi kuwalinda Wakenya huku akitoa onyo kwa wale waliokuwa wakichochea mapigano baina ya koo Transmara.

Naibu Rais Rigathi Gachagua, alieyandamana naye alisema utawala wa Kenya Kwanza utawanyamazisha wakosoaji wake kwa kuimarisha uchumi wa nchi hii.

“Nilisema pale Kasarani tulirithi serikali iliyoharibika lakini ndani ya mwaka mmoja Rais amefanya kazi usiku na mchana na tumeanza kuona matokeo, wiki iliyopita mliona bei ya mafuta ilishuka lakini watu waliokuwa wakilalamika sasa hawasemi hilo,” Bw Gachagua alisema.

Viongozi wengine walioandamana na Rais katika ibada ya mazishi ni pamoja na Spika wa Bunge la Kitaifa Moses Wetagula, Mawaziri Soipan Tuya (Mazingira) na mwenzake wa Barabara Kipchumba Murkomen.

Gavana wa Narok Patrick Ole Ntutu aliitaka jamii ya Maa kuishi kwa amani na kukomesha vita kati ya koo ambazo, akizitaka zitekeleze maendeleo.

Marehemu alitajwa kuwa ni mama mwenye bidii, mchapakazi na mwenye huruma nyingi kwa jamii.

 

  • Tags

You can share this post!

Afisi za uhamiaji Bungoma kuanza kutoa huduma kamili za...

Wamuratha aandaa timu ya wanawake 100 kunasua vijana kwa...

T L