Ruto ashangaza Wakenya ‘kukutana na marehemu’ Cheluget kujadili ardhi inayozozaniwa
KAULI ya Rais William Ruto kwamba alikutana na marehemu aliyekuwa Kamishna wa Mkoa wa Nyanza, Isaiah Kiplangat Cheluget kujadili uuzaji wa ardhi, imezua mshangao.
Akizungumza katika eneo la Sogoo, Narok, siku ya Jumatano, Rais Ruto alitangaza kuwa serikali iko kwenye mazungumzo na Cheluget kuhusu ununuzi wa shamba lenye ukubwa wa ekari 5,800 ili kuwapa makao watu waliotimuliwa kutoka msitu wa Mau.
Katika hotuba yake, Rais alitoa kauli ya kushangaza akisema alimwita marehemu Cheluget, akaketi naye na kuzungumza kuhusu ununuzi wa shamba hilo ili igawiwe wanaoidai.
“Tumemwita Cheluget na tumezungumza naye kuhusu ununuzi wa ardhi hiyo na serikali ili kuwapa wanaoidai,” alisema Dkt Ruto akiwa Sogoo siku ya Jumatano.
Mzee Cheluget alifariki Juni 26, 2017 katika Hospitali ya Aga Khan, Kisumu baada ya kuugua kwa muda mfupi na alizikwa nyumbani kwake Litein, eneobunge la Bureti, Kaunti ya Kericho, kabla ya kurudishiwa shamba hilo lenye rutuba.
Jaribio la kupata maoni rasmi kutoka kwa familia kuhusu mazungumzo hayo halikufua dafu kwani mmoja wa wanawe alisema hawapo tayari kujadili suala hilo hadharani kwa sasa.
Kwa zaidi ya miaka 15 sasa, familia hiyo imekuwa ikipambana na kesi kadhaa – ambazo imekuwa ikishinda mara kwa mara – kutoka Mahakama Kuu hadi Mahakama ya Rufaa dhidi ya wakazi 600 wa awali waliovamia shamba hilo kinyume cha sheria.
Licha ya kushinda kesi hizo, familia hiyo haijafaulu kurudishiwa shamba hilo kutokana na uhasama wa wakazi waliopo.
“Wakazi hao walitufukuza kwa nguvu, wakagawanya shamba hilo na kujenga majengo mwaka 1999 na 2000. Waliiba mali, wakaharibu baadhi ya vitu shambani na kuondoa mifugo, wakiwafukuza wafanyakazi,” alisema Bw Johnstone Kipkoech Langat, mwana mkubwa wa marehemu Cheluget, katika mahojiano ya hivi karibuni na Taifa Leo.
Bw Langat alisema “uvamizi huo ulianzisha mapambano ya kisheria ambayo tumeshinda mara tatu, ikiwemo Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufaa. Mahakama zote zimesisitiza kuwa ardhi hiyo ni ya marehemu baba yetu (Cheluget).”
Mnamo Juni 11, 2024, Mahakama Kuu ilitupilia mbali kesi iliyowasilishwa na wakazi hao 600 waliokuwa wakijaribu kuhalalisha umiliki wa ardhi hiyo kinyume cha sheria.
Jaji Mbogo Gitonga wa Mahakama ya Mazingira na Ardhi alitupilia mbali kesi ya Charles Kones kwa niaba ya wakazi hao akisema hawana haki ya kisheria kudai ardhi hiyo, ambayo kihalali ni mali ya marehemu Cheluget.
Wakazi hao 600 walikuwa wakitaka hati miliki hiyo ifutwe, waruhusiwe kuingia kwenye shamba hilo, kuligawa na kupimiwa sehemu walizonyakua pamoja na maeneo ya huduma za umma na kupatiwa hati miliki mpya.
Bw Johnstone Kipkoech Langat, Julius Kipkirui Langat, Laurence Kimutai Langat – kama wawakilishi wa marehemu Cheluget –, Msajili wa Hatimiliki Mchora Ramani wa Kaunti ya Narok, na Mwanasheria Mkuu walitajwa kwenye kesi hiyo kama washtakiwa.
Gavana wa Narok, Patrick Ole Ntutu, alisema juhudi za Rais kuwapa makazi wakazi wa Mau ni za kupongezwa kwani zitamaliza mzozo huo wa muda mrefu.
“Tunashukuru kuwa umetaja hali ya shamba la Cheluget kwani lina shule na familia. Kwamba umeanza mazungumzo ya kununua shamba hilo ni hatua nzuri,” alisema Bw Ntutu.
Familia zinazoishi katika shamba hilo zimezuia familia ya Cheluget kuingia au kulitumia, jambo ambalo Rais sasa amesema lazima limalizike kufikia mwisho wa mwaka.