• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Ruto asisitiza kusafisha mahakama ni lazima

Ruto asisitiza kusafisha mahakama ni lazima

NA BENSON MATHEKA

RAIS William Ruto ameapa kuwakabili na kuwaondoa majaji anaodai wanapokea hongo kuhujumu mipango ya serikali yake akisema atatumia “mbinu aliyoahidi” kushughulikia wanaolemaza ajenda zake kwa raia.

Licha ya kushutumiwa vikali kwa kuapa kukaidi maagizo ya mahakama, Dkt Ruto alisema hatakubali mipango yake iyumbishwe na maafisa wachache fisadi wa mahakama.

Kiongozi wa nchi alisema anaamini kuna majaji wengi wazuri katika mahakama lakini akasisitiza kuna wachache wanaopokea hongo ili kuhujumu mpango wake wa kuleta mageuzi ya kiuchumi nchini.

Mnamo Alhamisi alipuuza ushauri wa wanasheria waliomkashifu kwa kutisha na kuingilia uhuru wa mahakama akisema, kupitia X (iliyokuwa Twitter), kwamba “mambo ya wafisadi wote ni yale nilisema….”.

Rais Ruto amekuwa akionya wanaovuruga ajenda zake kwamba wataenda jela, wahame Kenya au wasafiri kwenda mbinguni.

Akijibu ujumbe wa Wakili Mkuu (SC) Ahmednassir Abdullahi aliyemtaka kukabiliana na maafisa fisadi wa mahakama, Rais Ruto alisema lazima majaji wote wanaopokea hongo waondolewe.

“Ulinionya kwamba nitahujumiwa na maafisa fisadi wa mahakama. Nilikwambia kuna maafisa wengi wazuri katika mahakama na kwamba tutawaondoa wale fisadi. Tutafanya hivyo,” alisema.

Rais Ruto alisema hayo licha ya wanasheria kupitia chama chao cha LSK, pamoja na Majaji na Mahakimu kupitia chama chao (KMJA), na Tume ya Huduma ya Mahakama (JSC) kupitia Jaji Mkuu Martha Koome, kumtaka awasilishe ushahidi alio nao kuhusu majaji fisadi ili wachukuliwe hatua za kisheria.

Eric Theuri

“Rais anafaa kufuata njia za kisheria kuwasilisha malalamishi yake dhidi ya maamuzi asiyoyapenda,” alisema Rais wa LSK, Eric Theuri.

Hata hivyo, Rais Ruto, kupitia msemaji wa Ikulu, Hussein Mohammed, alionekana kuwapuuza akisisitiza kuwa hataruhusu majaji kutumiwa kulemaza ajenda zake za maendeleo kwa Wakenya.

Hata hivyo, kiongozi wa nchi hakutaja mbinu atakayotumia kusafisha uozo anaodai umekolea katika mahakama.

Mnamo Januari 4, 2024, Rais Ruto aliendelea kushutumiwa kwa kuingilia uhuru wa mahakama, huku washirika wake wa kisiasa wakiendelea kumuunga mkono.

Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa, Kimani Ichung’wah alisema ni lazima majaji fisadi wa Mahakama Kuu waondolewe.

Bw Ichung’wah aliashiria uwezekano wa kufanyika mageuzi makali katika mahakama sawa na yaliyofanyika chini ya utawala wa Rais Mwai Kibaki akihudumu katika muhula wake wa kwanza mamlakani ili kuwaondoa majaji wafisadi na maafisa wengine wakuu katika mahakama.

Serikali ya marehemu Kibaki iliunda jopo lililowapiga msasa majaji ambalo lilipendekeza kutimuliwa kwa waliohusishwa na ufisadi.

Akizungumza katika mahojiano ya kipekee na Taifa Leo, Bw Ichung’wah alisema kuwa hivi karibuni viongozi wa Kenya Kwanza watajikita katika kuzidisha vita dhidi ya ufisadi.

Alieleza kuwa vita dhidi ya ufisadi vinalenga watu fisadi katika mihimili yote mitatu ya serikali.

Tume ya Kimataifa ya Wanasheria (ICJ), utanzu wa Kenya, ilimtaka Rais Ruto kuondoa matamshi yake yanayoonekana kutisha majaji na kuingilia Mahakama.

Mwenyekiti wa ICJ Kenya, Protas Saende alikashifu matamshi hayo akisema yanahujumu uadilifu na uhuru wa idara ya mahakama.

Aliongeza kuwa pia yanaweka hatarini utawala wa sheria wa nchi hii na uhuru wa mahakama.

“ICJ Kenya inamtaka rais kuondoa vitisho dhidi ya mahakama na kutoa taarifa ya kufafanua na kuthibitisha kujitolea kushikilia kanuni za uhuru wa mahakama na utawala wa sheria,” Saende alisema katika taarifa.

ICJ iliwataka maafisa wa serikali kushirikiana kushughulikia masuala yanayozuka bila kuathiri uadilifu wa mahakama.

  • Tags

You can share this post!

Kusitishwa kwa ujenzi wa barabara ya Sh30bn kulivyozima...

Waathiriwa wa mafuriko wataabika baada ya kambi kufungwa

T L