Habari za Kitaifa

Ruto atafika kortini kutoa ushahidi dhidi ya mwanafunzi aliyemkosea heshima?

Na RICHARD MUNGUTI March 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

MKURUGENZI wa Mashtaka ya Umma (DPP) Renson Ingonga hajaamuru kufutiliwa mbali kwa kesi ambapo mwanafunzi wa chuo kikuu ameshtakiwa kuchapisha habari za uwongo kuhusu Rais William Ruto, mahakama imeelezwa.

Wakili wa serikali Sonia Njoki alimweleza hakimu mwandamizi mahakama ya Milimani Benmark Ekhubi Jumatano, Machi 19, 2025 kwamba hajapokea maagizo kutamatisha kesi inayomkabili David Oonga Mokaya.

Mokaya ameshtakiwa kuchapisha katika mtandao wa kijamii picha ya Rais Ruto ndani ya jeneza ikiburutwa na Maafisa wa Jeshi kutoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee, Nairobi Hospital.

“Naomba kesi dhidi ya Mokaya itengewe siku ya kusikizwa kwa vile sijapokea maagizo kutoka kwa DPP niitamatishe,” Njoki alimweleza hakimu.

Kufuatia ufichuzi huo Bw Ekhubi aliagiza kesi hiyo ya kuchapisha habari za kupotosha na za uwongo isikizwe kuanzia Mei 29, 2025.

Mwanafunzi wa chuo kikuu David Oonga Mokaya (kulia)na Ian Mutiso wakiondoka mahakama ya Milimani baada ya kutajwa kwa kuchapisha habari za uongo kuhusu Rais William Ruto. PICHA|RICHARD MUNGUTI

Mokaya, ambaye ni mwanafunzi katika Chuo kikuu cha Moi alishtakiwa kwa kuchapisha habari za uwongo kwa kusambaza katika ukurasa wake wa X, “Landlord @bozgabi”, picha ya Rais ikiwa ndani ya jeneza ikiburutwa kwa landrover maalum kutoka chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee mnamo Novemba 13, 2024.

Mawakili Danstan Omari na Ian Mutiso waliandikia DPP atafakari upya uamuzi huo wa kumshtaki Mokaya wakitaka kujua ikiwa Rais Ruto ni miongoni mwa mashahidi.

“Bado hatujapokea majibu kutoka kwa DPP ikiwa rais ni mmoja wa mashahidi na kama ameandikisha taarifa ya ushahidi,” Bw Mutiso alimweleza hakimu Jumatano (Machi 18, 2025.)

Mabw Mutiso na Omari walitaka rais afike kortini kutoa ushahidi dhidi ya Mokaya.

Pia, Njoki alieleza mahakama taarifa za mashahidi hazijajumuisha ushahidi wa Rais Ruto.

Kufuatia ufichuzi kwamba DPP hajaamuru kesi itamatishwe, sasa Mokaya atakutana uso kwa uso na waliomfungulia malalamishi kwa mamlaka ya mawasiliano nchini CAK.

Mokaya amekana shtaka na yuko nje kwa dhamana.