Ruto ataka makanisa yashirikiane na serikali kukabili maovu katika jamii
WANDERI KAMAU NA PCS
RAIS William Ruto amesema kuwa Serikali na mashirika ya kidini yana jukumu la pamoja kushirikana kwenye juhudi za kukabili maovu katika jamii na kuziinua kiuchumi.
Rais Ruto alisema serikali itaendelea kushirikiana na makanisa ili kuboresha kiwango cha maisha cha Wakenya.
Akihutubu Jumanne Aprili 9, 2024, wakati wa Kikao cha 24 cha Baraza Kuu la Kanisa la PCEA, jijini Nairobi, Rais Ruto alieleza kuridhishwa kwake na jukumu linalotekelezwa na makanisa katika kuendeleza elimu, afya kati ya masuala mengine muhimu.
“Tunafurahia jukumu linalotekelezwa na makanisa katika masuala ya elimu, afya na kuihamasisha jamii kuhusu mambo tofauti,” akasema.
Rais alisema serikali itandelea kushirikiana na makanisa kuendeleza miradi ya maendeleo ili kuwasaidia raia.
Aliwaomba viongozi wa makanisa kuisaidia serikali kukabili pombe haramu, matumizi ya mihadarati na changamoto za ukosefu wa usalama zinazotokana na wizi wa mifugo.
Alieleza masikitiko yake kwamba familia nyingi zimeathiriwa na athari zinazotokana na matumizi ya pombe haramu na mihadarati, kwa sababu vijana wengi wana uraibu wa matumizi ya bidhaa hizo hatari.
Rais Ruto amekuwa akisisitiza kwamba serikali haitalegeza juhudi zake katika kukabili matumizi ya bidhaa hizo hatari kwa mustakabali wa vijana wengi.
Hata hivyo, Rais alikubali kwamba ukosefu wa ajira umechangia sana matumizi ya pombe na mihadarati.
Alisema vijana wengi wamekuwa wakijihusisha katika maovu hayo kwa kukosa jambo la kufanya.
“Hilo ndilo limetufanya kubuni mkakati kabambe kupitia mpango wa ujenzi wa nyumba na uchumi dijitali, ili kubuni nafasi za ajira miongoni mwa watu wetu. Kufikia sasa, kuna vijana 140,000 wanofanya kazi kwenye mpango wa ujenzi wa nyumba kote nchini,” akasema.