Habari za Kitaifa

Ruto ateua msajili mpya wa vyama vya kisiasa, mkuu wa KNCHR

Na JUSTUS OCHIENG August 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

Rais William Ruto ameteua maafisa wapya kuongoza Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa (ORPP) kufuatia kuondoka kwa aliyekuwa msajili, Anne Nderitu.

Katika uteuzi huo, John Cox Lorionokou amependekezwa kuwa Msajili mpya wa Vyama vya Kisiasa, huku Agatha Wanjiku Wahome akiteuliwa kuwa Msajili Msaidizi, uteuzi ambao unasubiri kuidhinishwa na Bunge la Taifa.

Bw Lorionokou ni afisa wa zamani wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC), na iwapo ataidhinishwa, atamrithi Sophia Sitati, ambaye kwa sasa anaongoza ORPP kama kaimu baada ya Bi Nderitu kuteuliwa kuwa Kamishna wa IEBC.

Wakati huo huo, Rais Ruto amemteua Claris Awour Onganga kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (KNCHR), kuchukua nafasi ya Roseline Odede aliyefariki Januari na ambaye nafasi yake ilikataliwa na Duncan Ojwang’ aliyeteuliwa awali.

“Rais amewasilisha rasmi majina ya walioteuliwa kwa Bunge la Taifa kwa kuzingatiwa na kuidhinishwa, kama inavyotakiwa kisheria,” alisema Hussein Mohamed, Msemaji wa Serikali, katika taarifa.

Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa ni taasisi muhimu katika demokrasia ya vyama vingi nchini Kenya. Inasimamia usajili, udhibiti, na ufadhili wa vyama vya kisiasa pamoja na kuhakikisha vinafuata masharti ya Sheria ya Vyama vya Kisiasa.

Ofisi hii pia imekuwa kitovu cha mizozo kuhusu uanachama wa vyama, makubaliano ya miungano ya kisiasa na ufuatiliaji wa sheria za uchaguzi, hasa kuelekea uchaguzi mkuu.

Uteuzi wa Bi Onganga umefanywa kufuatia mapendekezo ya Jopo la Uteuzi lililobuniwa kupitia Tangazo la Gazeti la Serikali Na. 4651 la Aprili 11, 2025.

Akiidhinishwa na bunge, Bi Onganga ataongoza KNCHR ambayo ina jukumu la kufuatilia, kuchunguza, na kuripoti kuhusu hali ya haki za kibinadamu, pamoja na kutoa ushauri kwa serikali kuhusu sera zinazozingatia haki.

Mwenyekiti wa KNCHR ana ushawishi mkubwa katika kuongoza mijadala ya kitaifa kuhusu haki, usawa, na utawala wa sheria.