Habari za Kitaifa

Ruto atinga miaka 3 mamlakani Wakenya wakisubiri atimize ahadi

Na MOSES NYAMORI, COLLINS OMULO September 10th, 2025 Kusoma ni dakika: 3

RAIS William Ruto ana miezi 24 tu kurekebisha makosa makubwa ya utawala wake na kutimiza ahadi zake nyingi alizotoa kwa Wakenya, ili aweze kutetea kiti chake mnamo 2027.

Akiwa amesalia na miaka miwili kabla ya uchaguzi mkuu wa 2027, Rais Ruto anakabiliwa na changamoto kubwa ya kutekeleza ahadi zake za 2022 za kuinua walio katika tabaka la chini, kuunda ajira kwa mamilioni ya vijana wasio na kazi, kuhakikisha huduma bora za afya na elimu kwa wote, pamoja na ujenzi wa maelfu ya nyumba za gharama nafuu.

Wakati wa kampeni, Rais aliahidi kuwa utawala wake utajengwa juu ya “demokrasia ya kikatiba, siasa za taasisi thabiti na kufungua milango ya fursa kwa wananchi wengi.”

Lakini miaka mitatu tangu aingie mamlakani, baadhi ya ahadi alizotumia kuwavutia Wakenya maskini bado hazijatimizwa.

Sasa analazimika kugeuza maneno kuwa vitendo, la sivyo aachwe akihesabiwa kuwa kiongozi aliyetoa maneno matamu bila matokeo.

Tangu kuapishwa Septemba 13, 2022, mfanyabiashara wa kuku aliyegeuka kuwa Rais amejipata katikati ya changamoto za kisiasa na kiuchumi, huku akikabiliwa na presha kubwa ya umma kuhusu ushuru wa juu na hali ngumu ya maisha.

Ushuru wa juu ni tishio kuu kwa utawala wake, hasa baada ya kupingwa kwa Sheria ya Fedha iliyopendekeza ushuru mpya, jambo lililosababisha maandamano ya kitaifa.

Rais amesisitiza kuwa ushuru ni muhimu kwa maendeleo, lakini hasira za wananchi kuhusu gharama ya juu ya maisha zinatishia azma yake ya kuchaguliwa tena.

Wafuasi wake wanasema anastahili muhula wa pili kutokana na miradi yake ya kuwanufaisha wananchi kama Hazina ya Hasla, Nyumba za gharama Nafuu, na Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA).

Wanadai Kenya Kwanza imeongoza nchi kupitia mfumuko wa deni, mabadiliko ya kiuchumi duniani, na imesaidia kuimarisha sarafu ya Kenya dhidi ya dola ya Amerika.

Hata hivyo, wakosoaji wake wanasema amewaongezea Wakenya mzigo wa ushuru huku akishindwa kuwazuia wandani wake wanaojivunia utajiri mkubwa kupitia miradi ya “uwezeshaji”, ilhali Wakenya wengi wanataabika kwa umaskini.

Pia, licha ya mfumuko wa bei kupungua, gharama ya maisha bado iko juu. Mageuzi katika sekta muhimu kama elimu na afya yamekumbwa na upinzani mkubwa, huku mfumo mpya wa ufadhili wa vyuo vikuu ukitajwa kuwa kikwazo kikuu.

Wakenya wanaopata mishahara wameona kipato chao kikikatwa kwa ushuru mpya ukiwemo: ushuru wa asilimia 1.5 wa ujenzi wa nyumba, asilimia 2.7 kwa Bima ya Afya ya Jamii (SHIF) na ongezeko katika michango ya NSSF.

Hatua hizi, pamoja na ushuru zaidi uliopendekezwa katika Mswada wa Fedha 2024, ziliibua maandamano makubwa ya vijana, yaliyopelekea Rais kukataa mapendekezo hayo.

Seneta Enoch Wambua wa Kitui alisema hata Rais mwenyewe anajua ameshindwa kutekeleza karibu kila ahadi aliyoitoa.
Kuanzia SHA, makazi nafuu, mfumo wa elimu hadi ununuzi dijitali, zote zimewakwaza wananchi.

Aliongeza kuwa usalama umedorora mno.

“Wakazi wa Kaunti ya Kitui watakuambia hali ni mbaya kuliko hata enzi za Shifta chini ya Kenyatta na Moi. Sasa majambazi wanatawala ovyo.”

Hata hivyo, Rais Ruto na wafuasi wake wanasisitiza kuwa bado wako kwenye mkondo wa kuinua maisha ya Wakenya
Katika manifesto yake, Rais Ruto aliahidi kujenga nyumba mpya 250,000 kila mwaka na kuongeza makazi ya gharama nafuu kutoka asilimia 2 hadi 50.

Lakini baada ya kuingia mamlakani, lengo hilo lilipunguzwa hadi nyumba 200,000 kwa mwaka. Hadi sasa, serikali inapaswa kuwa imejenga nyumba 600,000.

Katika kampeni za 2022, Ruto aliahidi kuboresha hali ya maisha kupitia uchumi wa kutoka mashinani hadi juu. Lakini bajeti yake ya kwanza iliyoanza Julai 1, 2023, ilileta ushuru mpya ukiwemo asilimia 16 kwa mafuta.

Msemaji wa Ikulu, Hussein Mohammed, anasema licha ya changamoto hizo “Rais Ruto amechukua hatua thabiti ambazo zimeimarisha uchumi. Pato la taifa (GDP) limefikia Sh 17 trilioni mnamo Mei 2025, huku mfumuko wa bei ukipungua kutoka asilimia 9.6 hadi asilimia 4.1.”

Lakini Profesa XN Iraki, mwanauchumi kutoka Chuo Kikuu cha Nairobi, anasema: “Uchumi unakua kwenye karatasi, lakini kwa mwananchi wa kawaida hali bado ni ngumu. Pesa zinazokatwa ushuru zinawanyima watu uwezo.”

Katika manifesto, Kenya Kwanza iliahidi kutoa Sh50 bilioni kila mwaka kwa biashara ndogo kupitia mikopo nafuu.

Rais Ruto alizindua Hazina ya Hasla Novemba 30, 2022, ikisambazwa kupitia simu.

Hadi sasa Wakenya milioni 26 wamekopa zaidi ya Sh 74 bilioni, Sh5 bilioni zimehifadhiwa kama akiba, Wakenya milioni 7 waliokuwa kwenye CRB wameondolewa, wakipata tena fursa ya mikopo.

Serikali ilianzisha Mamlaka ya Afya ya Jamii (SHA) kuchukua nafasi ya NHIF.

Licha ya watu kulipa michango ya kila mwezi hawapati huduma za kuridhisha huku hazina ikikumbwa na kashfa za ulaghai.