Habari za Kitaifa

Ruto awapa machifu jukumu la kufanikisha ajenda ya serikali

Na CECIL ODONGO December 2nd, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto ameonya kuwa serikali haitawavumilia viongozi ambao wanawatumia vijana kama wahuni, kusababisha ghasia, kuharibu mali na kuhatarisha maisha ya Wakenya.

Ili kukomesha tabia hiyo, Rais amemwamrisha Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja achukue hatua na kukabiliana na yeyote anayehusika katika uhuni au uchochezi akisema usalama wa nchi si suala la kuchezewa.

“Mazingira yaliyo salama ndiyo huwavutia wawekezaji na kusababisha nchi iendelee,” akasema Rais.

Alikuwa akiongea Jumatatu katika Chuo cha Mafunzo ya Polisi Embakasi, Nairobi wakati wa hafla ya kufuzu kwa machifu na manaibu wao.

Kiongozi wa nchi alisema Kenya itapiga tu hatua kiuchumi iwapo kutakuwa na usalama, uthabiti na uongozi unaofaa.

Aliwataka machifu na manaibu chifu watambue wezi wa mifugo, majahili na watu binafsi ambao wanatishia usalama wa kitaifa akisema wahalifu hawawezi kutamba wakati maafisa wa usalama wapo nchini.

Rais Ruto alisema mafunzo kwa zaidi ya machifu na manaibu chifu 6,000 yanaonyesha nia ya serikali ya kuhakikisha nidhamu na utaalamu katika sekta ya umma ili kuimarisha utoaji huduma mashinani.

Alisema machifu wana wajibu wa kuelimisha umma kuhusu mipango ya serikali ikiwemo elimu, nyumba za gharama nafuu, afya na kuhakikisha kuwa Wakenya wananufaikia miradi ya serikali.

“Mnatarajiwa kuelimisha umma kuhusu mipango ya serikali, kukanusha habari feki dhidi ya serikali, kulinda ardhi ya umma na kuunga mkono miradi ya ujenzi wa nyumba,” akasema.

Alisema machifu na manaibu wao wamechangia idadi ya wakulima waliosajiliwa kupanda kutoka 300,000 hadi milioni 7.1.

Pia alisema wameshirikiana na maafisa wa afya wanaohudumu nyanjani kuhakikisha zaidi ya Wakenya milioni 27 wanasajiliwa katika Bima ya Afya (SHA).

Aliongeza kuwa maafisa wote wa utumishi wa umma, watahitajika kupitia mafunzo ndani ya miezi sita ya kuajiriwa ili kuimarisha utendakazi wao.

Vilevile, kiongozi wa nchi alitangaza mpango wa serikali wa kupambana na matumizi ya dawa za kulevya, unywaji wa pombe haramu huku akisema kuwa kuna haja ya kuwalinda waathiriwa wa dhuluma za kijinsia.