• Nairobi
  • Last Updated May 5th, 2024 3:08 PM
Ruto akataa ‘kukaliwa chapati’

Ruto akataa ‘kukaliwa chapati’

BARNABAS BII Na STANLEY KIMUGE

RAIS William Ruto amesema yuko tayari kufanya mazungumzo na nguzo nyingine mbili za serikali ambazo ni mahakama na bunge, kwa lengo la kumaliza mvutano kuhusu ufisadi, kila upande kujitafutia masilahi ya kibinafsi, pamoja na kile alidai ni kuhujumiwa kwa utawala wake. 

Kiongozi wa nchi ambaye Jumanne alikuwa katika eneo la Tinderet, Kaunti ya Nandi, alisema yuko tayari kuongoza mazungumzo hayo, lakini akisisitiza haja ya kuwepo kwa Jaji Mkuu Martha Koome na Maspika Moses Wetang’ula (Bunge la Kitaifa) na Amason Kingi (Seneti).

“Mnamo Jumatatu, Jaji Mkuu aliomba tufanye mazungumzo na ninasema kwamba ninakubali yafanyike. Mnamo Januari 2, 2024, nilitangaza kwamba mjadala unafaa kufanyika wa namna ya kukabiliana na jinamizi la ufisadi ambalo linahujumu mipango ya serikali ambapo makateli hawataki tubadilishe taifa hili,” akasema Rais Ruto.

Dkt Ruto pia alisema mwaka 2024 ni wa kutokomeza ufisadi serikalini, masilahi ya kibinafsi ya baadhi ya maafisa serikalini na utepetevu.

Rais alizindua miradi kadhaa ya maendeleo na kuahidi mpango wa afya wa serikali ya Kenya Kwanza unalenga kuwanufaisha wengi katika jamii.

“Tunataka kukabiliana na makateli wasiotaka tulete mabadiliko nchini, watu wasiotaka kuona kila Mkenya akipata huduma bora za afya au kina mama mboga na wahudumu wa bodaboda wakimiliki nyumba. Hatutakubali watu hao kuishika serikali mateka kupitia utoaji hongo kwa majaji na kutafuta huduma za mawakili ghali,” akasema.

Kiongozi wa nchi alikuwa ameandamana na Naibu Rais Rigathi Gachagua, Gavana wa Nandi Stephen Sang, masenata Samson Cheragei (Nandi), Jackson Mandago (Uasin Gishu), Kiongozi wa Wengi katika Bunge la Kitaifa Kimani Ichung’wah na wabunge kadhaa wakiwemo Mbunge Mwakilishi wa Kike wa Nandi Cynthia Muge, Paul Biyego (Chesumei), Julius Melly (Tinderet), Marryane Kitanny (Aldai), Abraham Kirwa (Mosop), Josses Lelmengit (Emgwen), na Julius Kitur (Nandi Hills).

Mnamo Jumatatu Jaji Mkuu aliitisha mkutano baina ya asasi ya mahakama na Rais Ruto kutatua mkwamo na mkwaruzano unaoshuhudiwa kwamba ufisadi umekolea mahakamani.

Rais Ruto na viongozi wengine wa Kenya Kwanza kwa muda mrefu, wamekuwa wakitoa matamshi ya kuishambulia mahakama, wakidai kuna baadhi ya watu wanaowatumia majaji mafisadi kukwamisha miradi ya serikali kama vile nyumba za bei nafuu na mpango mpya wa bima ya afya.

[email protected]  [email protected]

  • Tags

You can share this post!

Samatta asema Taifa Stars ya TZ iko tayari kuizima Morocco

Ombi la kutimua Jaji Esther Maina lawasilishwa JSC

T L