• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 7:50 AM
Ruto kufadhili kampeni ya Raila kutwaa uenyekiti AUC

Ruto kufadhili kampeni ya Raila kutwaa uenyekiti AUC

NA JUSTUS OCHIENG

SERIKALI inapanga kuanzisha afisi na kutenga bajeti ya kumsaidia kiongozi wa Azimio la Umoja One Kenya Raila Odinga katika kampeni yake ya kuwania uenyekiti wa Tume ya Muungano wa Afrika (AUC).

Bw Odinga anatarajiwa kuwasilisha rasmi maombi yake kwa wadhifa huo Aprili 15, 2024.

Kampeni za wadhifa wa hadhi ya kimataifa kwa kawaida huhitaji uwekezaji mkubwa wa kidiplomasia, usafiri na matangazo; shughuli ambayo inagharimu pesa nyingi.

Mnamo 2017, Kenya ilitumia Sh437.7 milioni kumpigia debe aliyekuwa waziri wa mashauri ya kigeni Amina Mohamed.

Taifa Dijitali imebaini kuwa afisi inayoanzishwa na serikali na wanamikakati wa Bw Odinga kuendesha kampeni zake, itakuwa kitovu cha shughuli zake zitakazoshirikisha ofisi ya Rais, Odinga binafsi na kikosi chake, Wizara ya Mashauri ya Kigeni na Wakenya wanaoishi ng’ambo na vile vile mawaziri wa mashauri ya kigeni wa mataifa ya Afrika Mashariki.

Kikosi cha kampeni cha Bw Odinga kimebuni mikakati yenye awamu tatu ambazo ni za “Mkakati wa muda mfupi, mkakati wa kati na mkakati mkuu” kabla ya uchaguzi utakaofanyika Februari 2025.

Aliyekuwa Balozi wa Kenya nchini Amerika Bw Elkanah Odembo ambaye ni mmoja wa wanamikakati wa Bw Odinga anayeshirikiana na serikali kufanikisha kampeni za waziri mkuu huyo wa zamani, Jumapili, Machi 24, 2024 alithibitisha kwamba “afisi kamili itaanzishwa na bajeti ya kutosha inaandaliwa.”Bw Odembo hakuweza kufichua mengi kuhusu bajeti kamili ya kampeni hizo akisema “afisi na bajeti ni mada za mkutano unaopangwa kufanyika wiki hii”.

Balozi huyo wa zamani alieleza kuwa mkakati wa awamu tatu ambao umeundwa unahusu muda mfupi wa kati ya wiki nne na sita ambao lengo lake ni kuomba uungwaji mkono wa marais 16 wa nchi na serikali katika ukanda wa Afrika Mashariki.

“Lengo la mkakati wa kati kutoka Julai hadi Agosti 2024 ni kutafuta uungwaji mkono na kuidhinishwa na wakuu wengine wa nchi na serikali za kanda za Kusini, Magharibi, Kaskazini na Kati,” Bw Odembo aliambia Taifa Dijitali kupitia mahojiano.

Mkakati mkuu, ambao alisema ni mpango wa kuzoa ushindi “unahusu ofisi ya rais kuwasiliana na marais na wakuu wa serikali kuomba waunge Kenya na Bw Odinga kutembelea kila rais na kiongozi wa serikali kupata baraka zao”.

Rais Ruto, Bw Odinga na maafisa wa ngazi za juu wa wizara ya Mashauri ya Kigeni wakiongozwa na Mkuu wa Mawaziri, Musalia Mudavadi na Katibu Dkt Korir Sing’oei wamekuwa na shughuli nyingi kukutana na marais wa ukanda huu kuwaomba wamuunge Bw Odinga.

“Lengo letu kuu ni kushinda uchaguzi huu Februari 2025 katika raundi ya kwanza, ikiwa ni thuluthi tatu za nchi wanachama zinazostahili kupiga kura,” alisema Bw Odembo.

Alisisitiza kuwa uamuzi wa Baraza Kuu la Muungano wa Afrika kuthibitisha kwamba ni zamu ya Afrika Mashariki kuwasilisha mwenyekiti ajaye wa AUC, ulimuondolea kisiki Bw Odinga kugombea wadhifa huo.

“Uamuzi huu uliondoa kisiki kikubwa katika kampeni ya RAO na kuashiria kuanza kwa kampeni kamili. Kazi ngumu sasa inaanza,” akasema.

 

  • Tags

You can share this post!

HELB na KUCCPS kufutiliwa mbali kwenye mswada mpya

Mwanateknolojia na mwalimu stadi

T L