Ruto, Uhuru na Moi kukutana jukwaa moja kongamano kuhusu demokrasia Afrika
RAIS William Ruto, mtangulizi wake Uhuru Kenyatta na Mwenyekiti wa Kanu Gideon Moi watashiriki jukwaa moja wiki hii katika mkutano wa shirika la kutetea demokrasia Afrika, “Democracy Union of Africa” (DUA), jijini Nairobi, hatua inayoashiria mabadiliko yajayo katika ulingo wa siasa.
Mkutano huo ulianza jana na utaendelea hadi Jumatano, Oktoba 29, 2025 na kuhudhuriwa na aliyekuwa Rais wa Ghana, Nana Akufo-Addo.
Vilevile, mkutano huo utakaojadili hatima ya demokrasia barani Afrika, utahudhuriwa na jumla ya wajumbe 300 wakiwemo marais wengine wa zamani na sasa, watunga sera na wataalamu kutoka Afrika.
Utafanyika katika mkahawa wa Radisson Blu na baadaye katika Makao Makuu ya Kanu.
Mkutano huo unafanyika wakati joto limetanda katika anga ya siasa nchini Kenya, kufuatia tangazo la Rais Ruto kwamba Gideon Moi amejiunga na Serikali Jumuishi.
Dkt Ruto pia alithibitisha kuwa anafanya mazungumzo na Bw Kenyatta kama sehemu ya juhudi za kuleta maridhiano nchini kwa lengo la kupalilia umoja wa kitaifa na kuleta uthabiti katika serikali yake.
Kanu, ambayo ni mwenyekiti wa mkutano huo wa DUA, ilisema mkutano huo utajadili mustakabali wa Afrika chini ya kauli mbiu “Navigating Africa’s Position in a Multipolar World: Towards a Mutually Beneficial and Equitable Partnership.” (Nafasi ya Afrika katika Ulimwengu wenye ushindani: Kufanikisha Manufaa ya Mataifa yote na Ushirikiano Sawa).
Rais Ruto, Bw Kenyatta na Bw Moi – zamani wakiwa washirika na wakageuka mahasidi– sasa wataketi pamoja katika kile wachanganuzi wanasema ni ishara ya wao kushirikiana kisiasa.
Rais Ruto na Bw Kenyatta walikosana kuanzia Machi 2018, wakati wa muhula wao wa pili madarakani. Hatua hiyo ilichangia Ruto kujiondoa kutoka chama cha Jubilee na kuunda chama cha United Democratic Alliance (UDA).
Bw Moi, wakati huo akiwa mshirika wa Bw Kenyatta, baadaye alimuunga mkono marehemu Raila Odinga wa Azimio la Umoja-One Kenya katika uchaguzi mkuu wa 2022.
Bw Moi, ambaye ni Seneta wa zamani wa Baringo, ni mwanasiasa wa hivi punde wa upinzani kuridhiana na Dkt Ruto tangu mwaka jana.
“Kujumuishwa kwa Gideon Moi katika mazungumzo yanayoendelea kati ya Rais na rais mstaafu Kenyatta kunaonyesha kujitolea kwa serikali kupanua zaidi serikali ili kujumuisha washirika zaidi wa kisiasa,” akasema afisa mmoja wa Ikulu.
Akiongea kabla ya mkutano huo, Bw Moi alisema kuandaliwa kwa mkutano wa DUA nchini Kenya kunaiweka nchi hii katika nafasi bora ya mazungumzo kuhusu demokrasia.
“Kanu kuwa mwenyeji wa mkutano wa DUA 2025 jijini Nairobi, inaiweka Kenya katika kitovu cha ushirikiano wa kidemokrasia na kimataifa Afrika,” akasema Bw Moi.
“Mkutano huu utaleta pamoja baadhi ya viongozi wakuu Afrika kujadili siasa kama jukwaa la kuchanganua mawazo, ubunifu na ushirikiano,” mkurugenzi wa mawasiliano wa Kanu, Nyainda Manasse, akasema.
“DUA inaleta pamoja zaidi ya vyama 25 kutoka Afrika zinazoendeleza demokrasia, uhuru wa watu na utawala unaowajibika.
Mkutano huo ulianza jana kwa dhifa ya jioni ikifuatiwa na mkutano wa wajumbe leo, Jumatatu.