Habari za Kitaifa

Ruto ziarani TZ, Zimbabwe nyuma akiacha mafuriko, mgomo wa madaktari

April 26th, 2024 Kusoma ni dakika: 1

NA CHARLES WASONGA

HUKU taifa likizongwa na athari za mafuriko na mgomo wa madaktari, Rais William Ruto Alhamisi aliondoa nchini kwa ziara katika nchi za Tanzania na Zimbabwe.

Akiwa Tanzania Dkt Ruto anatarajiwa kuhudhuria sherehe za kuadhimisha Miaka 60 tangu Tanzania Bara kubuni Muungano na Kisiwa cha Zanzibar.

Kwenye taarifa aliyotuma kwa vyombo vya habari Alhamisi jioni Msemaji wa Ikulu Hussein Mohamed alisema: “Hatua ya Rais kuhudhuria sherehe hiyo ni kielelezo cha uhusiano mzuri, ujirani mwema, urafiki wa dhati na Jamhuri ya Umoja wa Tanzania na watu wake.”

Sherehe hiyo inafanyika Ijumaa.

Baada ya hapo, Rais Ruto ataanza ziara ya siku mbili nchini Zimbabwe.

“Ziara hiyo inalenga kuimarisha mahusiano ya kisiasa, kiuchumi na kijamii kati ya nchi hizo mbili,” Bw Mohamed akasema.

Akiwa Zimbabwe, Rais Ruto pia atakuwa mgeni mheshimiwa katika Maonyesho ya 64 ya Kimaitaifa ya Kibiashara ya Zimbabwe jijini Bulawayo.

“Akiwa katika mkutano huo, Rais anatarajiwa kusisitiza umuhimu wa maonyesho ya kibiashara kama kichocheo cha ukuaji wa kiuchumi, ustawi wa kiviwanda na uzalishaji wa nafasi za ajira,” Bw Hussein akasema.

Akiwa Zimbabwe, Ruto anatarajiwa kutia saini mikataba saba ya maelewano katika nyanja za afya, ulinzi, uwekezaji, elimu, uchukuzi na mafunzo katika utumishi wa umma.