Saa za kimbunga Hidaya kuwasili Kenya zakaribia
NA CHARLES WASONGA
IDARA ya Utabiri wa Hali ya Hewa nchini inasema kuwa kimbunga Hidaya kimewasili katika Pwani ya Tanzania huku kikitarajiwa kufika Pwani ya Kenya kuanzia Jumapili.
Kwenye taarifa Jumamosi, idara hiyo ilisema kimbunga hicho kitakachoandamana na upepo mkali pamoja na mvua kubwa, kinatarajiwa kuongezeka nguvu mnamo Jumatatu hadi Jumanne.
“Tayari athari za kimbunga hicho zimeanza kuonekana karibu na ufuo wa Bahari Hindi upepo ukivuma kwa kasi ya juu na mawimbi makubwa yakizidi urefu wa mita mbili,” taarifa hiyo ikaeleza huku ikiongeza kuwa inafuatilia hali hiyo.
Imewashauri wakazi wa maeneo ya pwani kuwa waangalifu, hawa wale wanaoendesha shughuli baharini kuzisitisha kwa muda hadi hali iimarike.
Wakati wa Hotuba yake kwa Taifa mnamo Ijumaa, Rais William Ruto alisema kimbunga Hidaya kitashuhudiwa nchini “wakati wowote” na akatoa wito kwa wakazi wa pwani kuwa waangalifu.
“Ripoti za idara ya utabiri wa hali ya anga zinatoa taswira hatari. Mvua itaendelea kunyesha kwa wingi kwa kipindi kirefu ndani ya mwezi huu wa Mei wote na hata mwezi ujao wa Juni,” akasema Dkt Ruto.
“Kimbunga Hidaya inatarajiwa kusababisha mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi mazito na makali ambayo huenda yakavuruga shughuli katika Bahari Hindi na makazi kando mwa Pwani ya Kenya,” Rais Ruto akaongeza.