Saba Saba: Wakazi wa Mavoko wahofia ghasia
HUKU wasiwasi ukizidi nchini kuhusiana na hofu ya ghasia wakati wa kuadhimisha siku ya Saba Saba Jumatatu, Julai 7, baadhi ya wakazi wa Athi River, Mavoko wanapinga mikutano ya hadhara ya kuadhimisha siku hiyo.
Wakizungumza mjini Athi River, Kaunti ya Machakos, Alhamisi, kundi la wakazi wanaoungana na chama tawala cha United Democratic Alliance (UDA) walilalamika kwamba maandamano ya kupinga serikali yaliyopita yameingiliwa na wahuni.
Boniface Mutinda, kiongozi wa vijana wa UDA, Mavoko, alisema kwamba pamoja na vifo vilivyotokea, maandamano hayo yameacha uharibifu mkubwa na wizi ambao unahatarisha usalama wa taifa.
“Kila tukio la maandamano tunaomba vifo na uharibifu wa mali. Tunawaomba vijana kubadili mbinu za kuwasilisha malalamishi yao. Vijana wa Mavoko hawatashiriki tena katika maandamano yoyote,” alisema Mutinda.
Walikiri kuwa tukio la Saba Saba la mwaka 1990 ni kumbukumbu muhimu ya demokrasia ya vyama vingi na utawala bora nchini, lakini wakasema kuwa hali ya sasa ya maandamano imejaa chuki na ghadhabu.
Wakiahidi kuwa waaminifu kwa serikali, wakazi hao wanahimiza Wakenya kueleza kutoridhika kwao kwa njia za amani.
“Tutaunga mkono serikali ya Kenya Kwanza. Tunangoja kwa hamu ziara ya Rais Ruto katika Ukambani hivi karibuni kufurahia manufaa ya serikali yake,” alisema Chris Mule, mwenyekiti wa chama cha UDA Mavoko.
Wakazi hao pia waliitaka serikali kutimiza ahadi zake, ikiwemo ahadi kwa wakazi wa Mavoko za kuwaruhusu kumiliki mashamba yaliyo na migogoro.
Katika ziara yake ya hivi majuzi Ukambani, Naibu Rais Kithure Kindiki aliwaahidi maskwota kuwa serikali itazingatia maombi yao ya kumiliki kisheria mashamba matatu makubwa.
Miongoni mwa maombi ya wakazi hao ni pia kupunguza bei za mashamba yanayouzwa na benki ya KCB na kampuni ya Portland Cement ambayo iko katika mchakato wa kuweka mipaka halali, huku usalama ukihatarishwa na magenge ya wahalifu.
“Mizozo ya umiliki wa ardhi Athi River inahitaji suluhisho la kisiasa na nia njema ya serikali. Eneo la Ukambani limekuwa likipinga serikali kwa miaka 17 sasa. Sasa tutasaidia serikali na kufurahia faida zake,” alisema Simon Muiya.
Wakazi wanasema wanategemea kauli za Naibu Rais Kindiki huku wakiahidi kuunga mkono serikali ya Rais Ruto. Katika wiki mbili zilizopita, Kindiki alifanya ziara katika ngome ya chama cha Wiper mikutano iliyovutia umati.