Saba wafariki katika ajali ya magari sita na pikipiki eneo la Mai Mahiu
WATU saba wameaga dunia katika ajali iliyohusisha magari sita na pikipiki eneo la Mai Mahiu katika barabara ya Narok – Nairobi.
Kulingana na polisi, magari sita yalihusika katika ajali hiyo ya saa nne asubuhi Jumatatu.
Kaimu Kamanda wa Kaunti ya Narok John Momanyi hakubainisha moja kwa moja idadi ya waliojeruhiwa.
“Ajali ilitokea wakati trela iliyokuwa ikisafiri kutoka Narok kuelekea Mai Mahiu ilipasuka gurudumu,” akasema Bw Momanyi.
Alisema trela hiyo iligonga gari aina ya Toyota Premio na basi la kampuni ya Ena Coach.
“Abiria watatu wa matatu walifariki papo hapo eneo la Duka Moja na Nairegia Enkare,” akafichua Bw Momanyi.
Wawili waliosafiri katika Toyota Prado walifariki papo hapo huku msafiri wa tatu akiaga dunia akipokea matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok.
“Trela ya pili iligonga pikipiki na kuua abiria wawili papo hapo,” Bw Momanyi akaeleza.
Magari yote yaliyohusika katika ajali pamoja na pikipiki zilipelekwa katika Kituo cha Polisi cha Ntulele.
Hadi wakati wa kuchapishwa kwa habari hii, majeruhi, ambao idadi yao haikubainika, walisafirishwa hadi Hospitali ya Rufaa ya Kaunti ya Narok kwa matibabu.
Ajali hiyo ilisababisha msongamano mkubwa wa magari kwa saa kadhaa huku polisi wakiwa na kazi ngumu kuondoa magari yaliyoharibika.
Bw Momanyi aliomba madereva wawe waangalifu na wafuate sheria za barabarani kuepuka ajali hasaa msimu wa Krismasi na mwaka mpya.